Watu nane ambao ni waombolezaji feki wanashikiliwa na polisi nchini Kenya kwa kudanganya kuwa walikuwa wanakwenda msibani, lengo lao likiwa ni kukwepa sheria za kudhibiti virusi vya corona jijini Nairobi.
Watu hao walinunua jeneza na kuliweka juu ya gari, na waliposimamishwa na polisi walisema wanasafirisha mwili wa marehemu kwenda Homa Bay kwa ajili ya mazishi na walikuwa wakitumia kibali cha kughushi cha mazishi.
Hata hivyo uongo wao ulibainika baada ya majirani wa eneo walilokuwa wanakwenda kukusanyika pamoja na wasifiri hao kwa ajili ya kuomboleza, walipoomba jeneza kufunguliwa ili wauone mwili wa aliyefariki, ndipo walibaini kuwa lilikuwa tupu.
Majibu ya vipimo vya corona yameonesha kuwa dereva wa gari hilo ana maambukizi ya virusi hivyo, na sasa wengine wamewekwa karantini, huku polisi wakiendelea na uchunguzi kubaini watu waliokaribiana na wasafiri hao kutoka Nairobi hadi Homa Bay.
"Hulka hizi za Wakenya zinanivunja moyo sana, sasa mtu ametoa coronavirus hapa na kupeleka Homa Bay. Tukisema watu wasitoke ni kwa ajili ya kutaka kukabili ugonjwa huu. Huu si ugonjwa wa serikali, ni wako na ni wangu," - Alisema jana Waziri wa Afya Kenya wakati akitoa taarifa hii