Na Issa Mtuwa – Ludewa
Timu ya Wataalamu Tisa kutoka Wizara Nne kwa ajili ya kwenda kumkwamua Mjasiriamali Rueben Mtitu maarufu Mzee Kisangani imewasili mkoani Njombe na kuripoti kwa Katibu Tawala wa Mkoa huo na baadae kuelekea wilayani Ludewa na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo
Andrea Tsere.

Ujumbe huo uliwasili mkoani Njombe juzi Aprili 03, 2020 wakitokea maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma, Dar es Salaam na Mbeya.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Prof. Silvester Mpanduji ambae ni Mkurugenzi Mkuu wa SIDO alimueleza DC kuwa Kamati yake ikiwa kwenye eneo la Mradi wa Mzee Kisangani itaainisha masuala mbalimbali ya Kiuchumi, Kibiashara, Kimazingira na Kijamii, huku ikibainisha viashiria hatarishi vinavyoweza kutokea kwenye mradi huo na namna ya kutatua.

Aliongeza kuwa wataalamu hao wako katika maeneo ya fani mbalimbali zitakazo kidhi kumkwamua Mzee Kisangani katika mradi wake kama serikali inavyokusudiwa. Kamati hiyo itaainisha masuala mbalimbali yanayohitaji katika kumsaidia Mzee Kisangani katika upanuzi wa mradi
wake.

Kila mjumbe anajukumu la kufanya na mara baada ya kazi hiyo ripoti ya kazi hiyo itawasilishwa kwa Waziri wa Madini Doto Biteko kwa hatua zaidi.

Kamati hiyo inatekeleza hadidu za rejea zilizotolewa na kikao cha mawaziri kilichokaliwa Machi 30, 2020 katika utekelezaji wa mpango kazi.

Uthubutu na ubunifu wa Mzee Kisangani umepelekea kumshawishi Waziri wa Madini Doto Biteko kuamsha hari ya kumsaidia Mzee Kisangani kutoka hali aliyonayo kibiashara na kufikia ndoto kubwa ya kuwa mfanyabiashara mkubwa huku akibainisha wizara yake kufanya kila linalowezekana kumwezesha kuwa mfanyabiashara mkubwa kupitia zana zake zinazotengenezwa na Madini ya Chuma.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Andrea Tsere, amemshukuru Waziri wa Madini Doto Biteko, kwa maamuzi ya kuundwa kwa timu hii huku akiwapongeza wataalamu hao kwa kuteuliwa kumsaidia Mzee Kisangani.

Ameongeza kuwa wilaya ya Ludewa ina Raslimali Madini za aina mbalimbali yakiwemo Chuma na Makaa ya Mawe huku kilio chake kikiwa ukosefu wa leseni za wachimbaji wadogo huku maeneo makubwa ya uchimbaji yakiwa yanamilikiwa na Shirika la Maendeo ya Taifa (NDC) huku akiwasilisha kilio hicho kwa mmoja wa Wajumbe kutoka (NDC) Dkt. Yohana Mtoni.