Serikali imetangaza rasmi kuwa wasafiri wote kutoka nchi zilizoathirika na ugonjwa wa virusi vya Corona, watalazimika kukaa Karantini kwa muda wa siku 14 katika hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es  Salaam maarufu hosteli za Magufuli.

Akizungumza katika hosteli za Magufuli, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema wasafiri hao watafikia katika hosteli za Magufuli ambazo zipo katika eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam.

“Lengo ni kuhakikisha tunadhibiti mienendo ya wasafiri hawa.Tumeona taarifa ambazo zimetoka kule Iringa, kuna baadhi ya wasafiri tuliwaweka hotelini wakatoroka sasa ili kudhibiti mienendo ya wasafiri hawa na kuwalinda Watanzania wengi tumeona kuna ulazima wa kuwaweka sehemu moja ambako kutakuwa na ulinzi wa saa 24 na mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Dar es Salaam,Bw. Paul Makonda atasimamia kwa karibu chini ya Wizara ya Afya,” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy Mwalimu amewataka wananchi kufahamu kuwa wasafiri hao si wagonjwa, bali ni kwa sababu wanatoka kwenye nchi zenye maambukizi yenye virusi vya Corona (Covid-19), hivyo hawapaswi kuchukuliwa kama ni wagonjwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameishukuru Wizara ya Afya kwa namna ambavyo imekuwa ikipambana kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Corona nchini. "sisi kama mkoa tumejipanga kuhakikisha kwamba watu wote wanaokuja na ambao wapo wanakuwa na afya njema kwa ajili ya kujenga uchumi wa mkoa wetu na Taifa kwa ujumla".

Makonda amewataka Watanzania kufanya kazi na kwamba kuanzia Jumatatu, Aprili 6 atawakamata wazururaji wote wanaozunguka mjini bila kuwa na kazi maalumu watakamatwa kwa kuwa wanasababisha mikusanyiko isiyokuwa na tija.