Wafungwa 44 wa kundi la wapiganaji wa msimamo mkali la Boko Haram waliokamatwa na jeshi la Chad mwanzoni mwa mwezi huu katika mkoa wa Lac wamekutwa  wamefariki dunia katika gereza usiku wa Alhamisi kuamkia Ijumaa wiki hii

Wafungwa hao walikabidhiwa mahakama siku ya Jumatano baada ya kukamatwa katika operesheni ya jeshi la Chad dhidi ya shambulio baya lililogharimu maisha ya askari wa chad katika moja ya kambi za jeshi la nchi hiyo.

Wafungwa 48 kutoka kundi la Boko Haram walizuiliwa katika kituo kimoja nje ya mji mkuu wa Ndjamena na kukabidhiwa mahakama siku ya Jumatano. Lakini Alhamisi asubuhi, 44 kati yao walikutwa wamefariki dunia katika  chumba walimo kuwa wamezuiliwa, kulingana na mamlaka ya Chad.

Kulingana na uchunguzi wa daktari, wapiganaji hao walikunywa sumu. Ripoti yake ya vipimo, kulingana na taarifa ya mwendesha mashtaka wa Ndjamena, Youssouf Tom, inaonysha kwamba walitumia vidonge vyenye sumu iliyosababisha  washindwe kupumua


Wote walikamatwa wakati wa operesheni iliyoitwa "Hasira ya Bohoma", iliyotekelezwa na jeshi la Chad kuanzia Machi 31 hadi Aprili 8. Karibu wanajeshi 52 wa Chadi na wapiganaji kadhaa wa Boko Haram waliuawa katika mapigano hayo


Credit:RFI