Wanajeshi wa Rwanda wadaiwa kuwabaka raia wakati wa amri ya kutotoka nje, Watano wadaiwa wakamatwa
Askari watano wa Rwanda wamekamatwa baada ya wakazi wa kitongoji cha mji mkuu wa Kigali kudai waliwabaka wanawake walipokua wakitekeleza sheria ya kukaa nyumbani iliyowekwa kote nchini humo ili kuzuwia mambukizi ya Covid-19, limesema jeshi la Rwanda.
Wakazi wa kitongoji cha Nyarutarama wameiambia ofisi ya mwendesha mashtaka wa jeshi pia kwamba askari waliwapiga wakazi na kuwaibia mali zao, kulingana na mwandishi wa BBC mjini Kigali.
Mmoja wa waathiriwa amewambia waandishi wa habari kuwa mnamo tarehe 26 Machi, mwanajeshi aliyekua amejihami kwa silaha aliingia kwa nguvu katika nyumba yake na kumpiga mume wake, na alipokua akijaribu kuingilia kati kumzuwia askari asimbake.
Serikali ya Rwanda iliweka sheria ya kutotoka nje kote nchini humo ili kuzuwia kusambaa kwa virusi vya corona, lakini baadhi ya wakazi wamekua wakilalamika juu ya ukatili wanaofanyiwa na maafisa wa usalama wanaosimamia utekelezwaji wa sheria hiyo.
Wiki iliyopita wanaume wawili walipigwa risasi na kuuawa walipopatwa wakitembea nje.
Polisi ilisema kuwa wanaume hao walijaribu kuwashambulia maafisa wa polisi
Rwanda imethibitisha visa 84 vya Covid-19.
Ramani ya Coronavirus: Kasi ya kusambaa kwa virusi 4 Aprili 2020
Maelezo haya yanatokana na data za mara kwa mara kutoka Chuo kikuu cha Johns Hopkins na huenda yasiangazie hali halisi ya mambo yalivyo katika kila nchi.