Rais wa Marekani Donald Trump amewaonya wamarekani kujitayarisha  kwa  idadi ya kutisha  ya  vifo vinavyotokana  na  virusi  vya  corona katika  siku  zijazo wakati  idadi  jumla ya  vifo  duniani  kote ikifikia 60,000.

Kesi zilizothibitishwa  na  wagonjwa wa  virusi  vya  COVID-19 nchini  Marekani  jana Jumamosi (04.04.2020) imepindukia  watu 300,000, lakini  Ulaya  inaendelea  kuadhibiwa na janga  hilo ambalo limesababisha  karibu nusu ya watu wote  duniani  kote  kujifungia ndani  ya  majumba yao kwa  gharama  kubwa ya  uchumi  wa  dunia.

Wagonjwa mahututi nchini Marekani waongezeka kutokana na virusi vya corona

Zaidi ya  vifo  vya  watu 45,000 duniani  kote  vimetokea  katika  mataifa  ya  Ulaya, ambapo Uingereza  imeripoti kiwango  cha juu  kipya cha  vifo  kwa  siku, na  kufikisha idadi  jumla  ya vifo  kuwa  4,300 kutoka  jumla  ya  kesi za  maambukizi 42,000.

Malkia Elizabeth wa pili atatoa  hotuba  maalum ya binafsi  leo Jumapili (05.04.2020) kuwataka  watu  kusimama  na  kupambana  na changamoto  hii  inayotokana  na  virusi  vya corona, na  binafsi  kuwashuruku wafanyakazi  wanaowahudumia  wagonjwa  wa  COVID-19.

Nina  matumaini  katika  miaka  inayokuja  kila  mmoja  ataweza  kujivunia  ni  kwa  njia  gani aliweza  kupambana  na  changamoto hii,” atasema  katika  hotuba  hiyo, kwa  mujibu wa vipande  vilivyotolewa  jana  Jumamosi.

Kwa hivi  sasa  kuna  zaidi  ya  kesi milioni 1.2 zilizothibitishwa  za  mambukizi  ya  virusi  vya corona  duniani  kote, na  kiasi  ya  watu 65,000  wamefariki  tangu  virusi  hivyo  vilipozuka nchini  China  mwishoni  mwa  mwaka  jana, kwa  mujibu wa  idadi  iliyojumlishwa  na chuo kikuu  cha  Johns Hopkins.

Trump  amesema  Marekani  inaingia  katika “wakati  ambao ni wa hali  ya kutisha” kwa “idadi  mbaya kabisa.”

“Hii  huenda  itakuwa  wiki  ngumu  kabisa,” alisema  katika  Ikulu  ya  White House. “kutakuwa  na  vifo  vingi sana.”

Wakati  huo  huo , rais  huyo  amesisitiza  kuwa  Marekani  haiwezi  kuendelea  kufungwa kwa milele.

“Mapambano dhidi  ya  virusi  ni  muhimu, lakini hatuwezi  kuiharibu  nchi  yetu,” amesema. “Nilisema  tangu  mwanzo , tiba haiwezi  kuwa  mbaya  kuliko  matatizo.”

The post Waliofariki kwa virusi vya Corona duniani wafikia 64,972 appeared first on Bongo5.com.