Idadi ya watu walioaga dunia kutokana na maambukizi ya virusi vya corona nchini Marekani imepindukia 42,518.


Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini humo imefikia 792,938  na kwamba 72,389 miongoni mwao wamepona

Kwa sasa Marekani inashika nafasi ya kwanza duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa virusi vya corona na vilevile kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wahanga wa virusi hivyo.

Kutokana na hali mbaya iliyosababishwa na ugonjwa wa Covid-19, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Marekani Rais wa Nchi hiyo Donald Trump ametangaza mkakati wa  "kulinda ajira" za Wamarekani. 

"Kwa kuzingatia shambulio la adui asiyeonekana, na kutokana na haja ya kulinda ajira za raia wetu wakuu wa Marekani, nitasaini agizo la rais la kusitisha kwa muda zoezi la kupokea wahamiaji nchini Marekani, "Trump ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mapema mwezi wa Januari, alizuia safari zozote kwenda China ambapo virusi vya Corona vilianzia mwezi wa Desemba mwaka jana, kabla ya kupiga marufuku safari kati ya Marekani na nchi nyingi za Ulaya katikati mwa mwezi Machi.