Kenya imetangaza kuwa na wagonjwa 246 wa corona baada ya kuthibitisha watu 12 wapya wameambukizwa virusi vya ugonjwa wa Covid 19. Katika taarifa waziri wa afya wa Kenya Mutahi Kagwe, amesema watano kati ya wale walioambukizwa virusi vya corona ni wahudumu wa hoteli na kuongeza kuwa idadi hiyo ilifikiwa baada ya jumla ya sampuli 400 kufanyiwa uchunguzi.
Hapo jana rais Uhuru Kenyata alitangaza hatua zifuatazo kukabiliana na Covid-19
- Wizara ya Afya na huduma za umma itaanzisha hazina ya kuwasaidia wafanyakazi wa Afya wanaokabiliana na mlipuko wa virusi vya corona
- Wizara ya elimu itachukua hatua kuwalinda wanafunzi kutokana na athari mbaya za hatua zilizochukuliwa kukabiliana na Covid-19
- Mamlaka ya usambazaji wa tiba nchini Kenya itaondoa masharti ya ununuzi wa vifaa vya kujilinda dhidi ya Covid-19 kwa takriban miezi mitatu ili kurahisishia kaunti kununua vifaa hivyo.
- Nyumba za watu wasiojiweza jijini Nairobi zitafaidi kutokana na fedha zilizotengwa na serikali kusaidia familia zisizojiweza
- Bunge litapitisha tena mapendekezo na miswada kuhusu vichocheo vya uchumi.
- Ili kuhakikisha msaada unagawanywa kwa njia salama, mfuko wa hali ya dharura wa kukabiliana na Covid-19, Kenya na mashirika mengine ya usalama yatashirikiana kuratibu miradi kama ule wa Adopt a Needy Family, ambapo raia wa Kenya wanasaidiana kipindi hiki cha janga kuhakikisha hatua zinachukuliwa bila kufuata urasimu
- Afisa yeyote wa polisi atakayekiuka sheria wakati anatekeleza hatua za kukabiliana na usambaaji wa virusi atakabiliwa na mkono wa sheria.
Upimaji
Kenya imepokea karibia vifaa 40,000 vya kupimia Jumatano ikiwa ni katika kuimarisha hatua za kuimarisha uwezo wa kupima watu kunakoendana na lengo la kupima, kutengwa walioathirika na kutibu.
Wizara ya afya imetangaza Jumatano kwamba nchi hiyo imepokea vifaa vya kupimia mfano wa vijiti 18,900, vifaa vya kuwekea vipimo 18,912, sare na vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya 3,790, vipimajoto vya kushikililiwa, glavu na mashine za kupuma kutoka kwa mfanyabiashara wa kundi la Alibaba, Jack Ma.
Waziri amesema Kenya pia ilikuwa imepokea shehena ya glavu, vifaa vya kujikinga kwenye uso na barakoa zinazovaliwa wakati wa upasuaji kutoka China, Ufaransa na Ujerumani kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO).
The post Walioambukizwa corona Kenya wafika 246, Wagonjwa wapya 12 appeared first on Bongo5.com.