Zaidi ya watu bilioni 4.5 wanaendelea kubaki majumbani kama sehemu ya juhudi zinazochukuliwa kwa hiari au za lazima ili kupunguza kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Marekani: Waandamanaji wapinga amri inayowalazimu kubakia majumbani (picture-alliance/dpa/E. Gay)

Japan, Mexico, Uhispania, Ufaransa, na Uingereza ni kati ya nchi ambazo zimeweka hatua hizo au hata kurefusha muda wa watu kubakia majumbani. Uswizi, Denmark na Finland zimetangaza kwamba maduka na shule zitafunguliwa tena kuanzia wiki ijayo.

Huko nchini Marekani, baadhi ya watu waliandamana ambapo walikuwa wanapinga amri ya kutotoka nje ambayo wanadai imeathiri uchumi wa nchi hiyo.

Waandamanaji wameonekana katika majimbo mbalimbali wakihitaji kufunguliwa kwa maeneo yao na watu waweze kuendelea na majukumu yao ya kila siku ili kuweza kunusuru hali ya uchumi.

Kesi za wagonjwa watokanao na virusi vya corona zinazidi kujitokeza katika majimbo mbalimbali nchini Marekani.

Rais Donald Trump ametangaza kuwa hatua hizo zitaanza kulegezwa katika majimbo ya Texas na Vermont kuanzia Jumatatu.

Ujerumani kwa upande wake imetangaza kuvidhibiti virusi hivyo baada ya watu 3,400 kufa kutokana na COVID -19 , na itaanza kulegeza baadhi ya hatua zilizowekwa kwa tahadhari kubwa. Baadhi ya maduka yameruhusiwa kufungua milango yake kuanzia Jumatatu, na baadhi ya watoto wataweza kurudi shuleni katika kipindi cha wiki moja ijayo.

Kwingineko Italia pia imeanza kupunguza makatazo na wakaazi mji wa Venice walionekana nje wakipunga hewa nje. Iran imeruhusu biashara kadhaa za mjini Tehran kufungua tena milango yake siku ya Jumamosi.

Dalili za kudorora kwa uchumi wa dunia unaosababishwa na janga la corona zinaendelea kujitokeza. China imetangaza kunywea pato la taifa la nchi hiyo kwa mara ya kwanza tangu kujitokeza hali kama hiyo mnamo miaka ya 90.

Vyanzo:/AFP/DW

The post Waandamana kupinga amri ya kubaki majumbani kisa Corona, Marekani appeared first on Bongo5.com.