Wazalishaji wakubwa wa mafuta ulimwenguni wamekubaliana kupunguza kiwango cha uzalishaji mafuta kwa takribani mapipa milioni 10 kwa siku ili kuidhibiti bei iliyoporomoka kutokana na janga la kirusi cha corona.
Waziri wa Mafuta wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman Al-Saud (kushoto) na mwenzake wa Urusi, Alexander Novak wakiongoza kikao cha OPEC mwezi Disemba 2019.
Katika mkutano wao kwa njia ya vidio siku ya Jumapili (13 Aprili), wazalishaji hao wa shirika la OPEC linalotawaliwa na Saudi Arabia na washirika wao wanaoongozwa na Urusi waliafikiana kukata 10% ya kiwango cha kawaida cha uzalishaji, ingawa katika uhalisia linaweza kufikia hadi asilimia 20.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nishati wa Mexico, Rocio Nahle, mataifa hayo yalikubaliana kuwa kuanzia mwezi Mei, yatazalisha mapipa milioni 9.7 ya mafuta kwa siku, chini kidogo ya mapipa milioni 10 iliyokuwa imezungumziwa awali.
Katibu Mkuu wa OPEC, Muhammad Barkindo, aliliita punguzo hilo kuwa la kihistoria.
“Ni kiwango kikubwa kabisa kwa ujazo na kirefu kabisa kwa muda, kwani kimepangwa kuchukuwa miaka miwili,” alisema na kuongeza kwamba makubaliano hayo yanafunguwa njia ya muungano wa kilimwengu na ushiriki wa mataifa ya G20.
Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman, ambaye aliongoza mkutano huo kwa kushirikiana na mawaziri wenzake wa Urusi na Algeria, alithibitisha kuwa mjadala wao wa siku nne ulimalizika kwa maridhiano.
Saudi Arabia inasema huenda punguzo hilo likakata uzalishaji wa mapipa milioni 12.5 kwa siku, kwa sababu ya kiwango kikubwa cha uzalishaji kutoka nchi hiyo, Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mazungumzo ya awali juu ya uzalishaji wa mafuta duniani yalikuwa yamekwama kutokana na mzozo na Mexico, lakini ufumbuzi ulipatikana baada ya mataifa wanachama wa OPEC kuliruhusu taifa hilo la Amerika Kusini kupunguza mapipa 100,000 tu kwa mwezi.
Trump afurahishwa na makubaliano
Rais Donald Trump wa Marekani aliyapokea makubaliano hayo aliyoyaita mazuri kwa wote, na ambayo yataokowa maelfu ya ajira kwenye sekta ya nishati nchini mwake.
“Ningelipenda kuwapongeza Rais Vladimir Pution wa Urusi na Mwanamfalme Muhammad bin Salman wa Saudi Arabia, ambao wote nimezungumza nao.” Aliandika Trump kwenye akaunti yake ya Twitter mara baada ya makubaliano hayo kutangazwa.
Ikulu ya Kremlin ilithibitisha kufanyika kwa mazungumzo kwa njia simu, ambapo Trump na Putin walikubaliana juu ya “umuhimu mkubwa” wa makubaliano hayo.
Canada pia imepongeza kufikiwa kwa makubaliano hayo, ambapo waziri wake wa rasilimali, Seamus O’Regan, ameandika kwenye Twitter kuwa sasa kutakuwa na “utulivu kwenye soko la mafuta ulimwenguni.”
Bei ya mafuta imeshuka tangu mwanzoni mwa mwaka kutokana na janga la COVID-19 kutokana na hatua za mataifa kadhaa kuzuia shughuli za kawaida za maisha, ambazo zimeshusha kiwango cha matumizi ya mafuta.
The post Virusi vya Corona vyaporomosha soko la mafuta duniani, mapipa milioni 10 kupunguzwa kuzalishwa appeared first on Bongo5.com.