Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema hivi karibuni atatangaza iwapo atalegeza masharti ya watu kukaa nyumbani kutokana na mamabukizi ya Corona, katika taifa hilo ambalo limeshuhudia maambukizi ya watu 79.

Wakati huo huo rais Yoweri Museveni ametangaza hatua mpya za kudhibiti mienendo ya madereva wa malori yanayoingia nchini humo kutoka mataifa jirani baada ya zaidi ya madereva 20 kupatikana na ugonjwa wa Covid-19.

Hatua hizo ni pamoja na kila lori kuwa na mtu mmoja - dereva pekee yake ambaye hataruhusiwa kulala hotelini wala nyumbani kwa watu.

Katika hotuba yake kwa taifa usiku wa Jumanne rais Museveni amebaini kwamba madereva hao ni tishio katika mapambano ya nchi hiyo dhidi ya Corona akitoa mfano wa janga la Ukimwi la miaka ya 1980 na miaka ya tisini wakati ambapo madereva wa malori katika kanda hiyo waliaambukiza watu virus vya HIV katika kila miji waliyopitia wakiwa safarini. Muda wa watu kubaki nyumbani unamalizika tarehe 5 Mei 2020.

Wakati hayo yakijiri Shirika la Kimataifa la Kutoa Misaada (IRC) limeonya kuwa watu bilioni moja huenda wakaambukizwa virusi vya Corona kote duniani, huku likisema nchi zisizojiweza zinahitaji usaidizi wa haraka.