Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma
Hadi sasa, Serikali imetenga jumla ya maeneo 46 katika sehemu mbalimbali nchini yenye ukubwa wa Hekta 281,533.69 kwa ajili ya kurasimisha wachimbaji wadogo.

Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma Waziri wa Madini Mhe.Dotto Biteko wakati akijibu swali la mbunge wa Msalala Mhe.Ezekiel Magolyo Maige aliyehoji kwa kuwa Serikali imekuwa ikiwarasimisha wachimbaji wadogo wa Madini:- a) Je, ni lini Serikali itawarasimisha Wachimbaji wadogo katika vijiji vya Busulwangili, Lwabakanga, Kakola namba Tisa na Wisolele katika Jimbo la Msalala; b) Je, ni sawa kwa mwenye leseni au msimamizi wa eneo la wachimbaji wadogo kupatiwa asilimia 30 ya mawe yanayochimbwa katika eneo lake.

 Katika Majibu yake Waziri wa Madini Mhe.Dotto Biteko amebainisha kuwa tangu mwaka 1996 Serikali kupitia Wizara ya Madini imekuwa ikitenga maeneo maalum kwa ajili ya kurasimisha wachimbaji wadogo wa madini nchini ambapo hadi sasa, Serikali imetenga jumla ya maeneo 46 katika sehemu mbalimbali nchini yenye ukubwa wa Hekta 281,533.69.

Aidha Mhe.Biteko amesema , Serikali itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kadri yatakavyokuwa yanapatikana ambapo katika Wilaya ya Kahama Serikali imeunda Kamati Maalumu ya utengaji wa maeneo kwa mujibu wa Kifungu cha 15 na 16 cha Sheria ya Madini Sura 123. 

Mhe. Biteko amefafanua kuwa kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuandaa utaratibu wa kugawa maeneo yote tengefu yakiwemo maeneo ya Kinamiyuba-Ilindi-Mwime, Buzwagi-Bumbiti na Nyangalata. Mpaka sasa jumla ya maombi 89 ya uchimbaji mdogo yamepokelewa na mchakato wa kugawa leseni hizo unaendelea. 

Pia amesema , Serikali kupitia Tume ya Madini imeifuta leseni ya utafutaji wa madini PL 8125/2012 iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni ya Liontown Tanzania Ltd iliyoko Kata ya Segese Halmashauri ya Msalala na eneo hilo linatarajiwa kutengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Waziri Biteko aliendelea kusema  kwa sasa maeneo ya Lwabakanga na Kakola namba Tisa yapo ndani ya leseni ya uchimbaji mkubwa SML 44/99 inayomilikiwa na mgodi wa Bulyanhulu Gold Mine Ltd hivyo, eneo hilo haliwezi kutengwa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji mdogo.

Aidha, eneo la Busulwangili lipo ndani ya leseni ya utafutaji wa madini PL 10782/2016 inayomilikiwa na Kampuni ya Hai Nan Geology (Tanzania) Co. Ltd. na  Serikali ipo katika hatua za awali za kufuta eneo hilo na kulitenga kwa ajili ya wachimbaji wadogo baada ya mmiliki wake kushindwa kufanya kazi ya utafiti.

Mhe.Biteko aliendelea kufafanua kuwa ,Serikali kupitia Tume ya Madini ilitoa Waraka wa Ndani Na. 3 ulioanza kutumika tarehe 15 Oktoba, 2019 wenye dhumuni la kutoa mwongozo kwa Maafisa Madini Wakazi na watumishi wengine katika kusimamia, kudhibiti shughuli za madini na mapato ya Serikali ambapo  Waraka huo unawataka wasimamizi kuzingatia ukusanyaji wa kodi za Serikali Kuu na Halmashauri na kuweka mgawanyo wa mapato baina ya mmiliki wa duara (mchimbaji), mmiliki wa shamba na msimamizi.

Hivyo,kwa Mujibu wa Waraka huo mgawanyo utazingatia kodi za Serikali Kuu na Halmashauri kwanza ambazo ni Mrabaha 6%, Ada ya ukaguzi 1% na Kodi ya huduma 0.3% na baada ya kutolewa kodi hizo, mmiliki wa ardhi atapata 15%, mmiliki wa Shamba 15% na mmiliki wa duara (mchimbaji) 70%.