Katika kipindi hiki cha kuelekea maadhimisho ya miaka 56 ya Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar, mimi kama Msimamizi Mkuu wa masuala yote ya Muungano napenda nitumie fursa hii kuzungumza machache na Watanzania wenzangu.

Moja; Nawapongeza Watanzania wote kwa kazi kubwa mnayoendelea kuifanya ya kuhakikisha Muungano wetu unazidi kuimarika siku hadi siku.  Vilevile niwapongeze kwa kuwa na imani thabiti juu ya Muungano wetu kwa kuhakikisha mnautunza na kuuenzi kwa hali na mali.

Kupitia Muungano huu, Watanzania tumeweza kudumisha Uhuru wa Tanganyika tulioupata mwaka 1961, na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964. Aidha, tumeweza kulinda na kuenzi yale yote tuliyoachiwa na waasisi wa Muungano wetu hususan Amani na Utulivu katika nchi yetu. Sote tunafahamu kuwa Amani na Utulivu ni kati ya vichocheo muhimu vya kukuza Uchumi, Ustawi wa Wananchi, na Maendeleo ya Taifa letu kwa ujumla.

Mbili; Napenda kuwakumbusha kuwa jukumu kuu la Muungano wetu ni kuhakikisha kuwa Mtanzania yeyote bila kujali umri, kabila, jinsia au dini anaweza kuishi, kufanya biashara na kufanya kazi upande wowote wa Muungano wetu bila bughudha yoyote. 

Muungano wetu unatoa fursa ya kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anajengewa mazingira mazuri ili apate haki yake ya kuishi. Haki hii ya kuishi imetiliwa mkazo na katiba za   Serikali zetu zote mbili - Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.  

Haki hii ni moja kati ya haki nyingine muhimu na imeainishwa katika Sura ya kwanza, Sehemu ya tatu, kifungu cha 14 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kinachosema; 
“Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria”. 

Kwa upande wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Sura ya tatu, kifungu 13 (1) na (2) kinasema ifuatavyo:

 13.-(1) Kila mtu anayo haki ya kuwa na hifadhi ya maisha yake. 

(2) Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria. 

Mbali na haki hii ya kuishi kulindwa na katiba zetu zote mbili bado kila mmoja wetu analo jukumu la kulinda uhai wake na uhai wa wanaomtegemea.

Tatu; Katika kipindi hiki ambacho nchi yetu inapitia kipindi kigumu cha kukabiliana na janga la maradhi yatokanayo na maambukizi ya virusi vya Korona (COVID 19), nichukue fursa hii kuwapongeza Watanzania kwa kuchukulia janga hili kwa uzito unaostahili pamoja na kuchukua tahadhari za kuhakikisha analinda maisha yake na wale wanaomtegemea.

Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa Serikali zetu zote mbili zitaendelea kulinda kikamilifu haki ya kuishi ya kila Mtanzania hususani katika kipindi hiki cha mlipuko wa mafua yanayosababishwa na virusi vya Corona kwa kuweka mipango madhubuti itakayohakikisha kuwa maisha ya Watanzania walio wengi hayapotei kutokana na ugonjwa huu. 

Niwaombe kila mmoja wenu kuwa mlinzi wa mwenzie kwa kuhakikisha kuwa mnatii na kukumbushana maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wetu wa afya.  Aidha niwasihi muongeze juhudi kuhakikisha kuwa mnajilinda na kulinda maisha ya wanaowategemea kwa kuepuka masuala yote yaliyotolewa tahadhari na wataalamu wetu wa afya kama vile kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.

Kabla ya kumalizia salamu zangu nichukue fursa hii kutoa pole kwa wale wote walioathirika kwa namna moja au nyingine kwa janga hili. Kwa wagonjwa wetu niwatakie nafuu ya haraka na kwa mlioondokewa na wapendwa wenu Mungu aendelee kuwafariji na kuwapa subira katika kipindi hiki kigumu na azilaze roho za marehemu mahali pema peponi amina.  

Watanzania wenzangu nafahamu maadhimisho haya hayana sherehe ila tutumie siku hii kujitathmini na kujipanga ni kwa namna gani kama taifa kwa pamoja tutakabiliana na janga hili la corona na kuhakikisha tunaweza kulitokomeza ili tuweze kurejea katika maisha yetu ya kawaida ikiwemo suala zima la kulinda Muungano wetu. Niwasihi kila mmoja awe mlinzi wa mwenzie kwani wahenga husema umoja ni nguvu utengano ni dhaifu. 

Hivyo nguvu za kila mmoja wetu ni muhimu na zinahitajika katika kukabiliana na ugonjwa huu. Niwatakie kila la kheri katika maadhimisho haya ya miaka 56 ya Muungano wetu, tuendelee kuusimamia na kuupigania Muungano wetu na kwa pamoja tutajenga taifa lenye ustawi.  Namuomba Mungu aibariki Nchi yetu, na atuondolee Mabalaa yote mbele yetu.

Mungu Ibariki Tanzania

Mungu Ubariki Muungano wa Tanzania

MUNGU WABARIKI WATANZANIA