Na WAMJW-SONGWE
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Breg. Jen. Nicodemus Mwangela ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe kuepuka misongamano katika maeneo yote, ikiwa ni moja ya njia ya kupambana na ugonjwa wa Corona usisambae endapo utaingia Mkoani hapo.

Ameyasema hayo, wakati akipokea vifaa vya kunawia mikono pamoja na vitakasa mikono kutoka Wizara ya Afya na Shirika la Project CLEAR, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya uhamasishaji kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona.

“Serikali imetoa maagizo mbali mbali, ambayo sisi kama Serikali ya Mkoa tunayasimamia na kuhakikisha yanatekelezwa, ikiwemo kusisitiza kuepuka msongamano na mikutano isiyokuwa yalazima katika maeneo mbali mbali na hili linatekelezwa vizuri kabisa” alisema.

Mbali na hayo, amesema kuwa, maambukizi ya ugonjwa wa Corona yameleta madhara makubwa kwa maisha ya binadamu hasa katika upande wa kiuchumi, huku akisisitiza kuwa nchi nyingi duniani zimeathirika kutokana na janga hili la Corona.

“Ni kweli kabisa huu ugonjwa sasahivi, umeleta madhara makubwa kwa Maisha ya binadamu, lakini pia kiuchumi, nan chi nyingi zenye uwezo mkubwa kiuchumi na kiafya zimeahirika kutokana na janga hili”alisema.

Aidha, Mhe. Alisema kuwa, Serikali inaendelea kutoa elimu na tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona kwa wananchi, hii inafuatia sababu kuwa, Mkoa wa Songwe upo mpakani mwa nchi za Malawi na nchi ya Zambia ambayo inapokea pia watu kutoka nchi ya DR Congo.

“Songwe ipo kwenye mlango, tusipotoa tahadhari ya kutosha kwa wananchi kuna hatari kubwa ya ugonjwa kuingia, Mkoa wa Songwe upo mpakani, tuna KM 135 tunapakana na Zambia, KM 45 tunapakana na Malawi, nchi zote hizo tayari zina maambukizi ya ugonjwa wa Homa kali ya mapafu, huku nchi ya DR Congo ikiongoza kuwa na wagonjwa wengi zaidi” alisema

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira kutoka Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima amesema kuwa katika kupambana na ugonjwa huo Serikali kupitia Wizara ya Afya inakabidhi vifaa vya kunawa mikono (sanitizer) lita 150 , Dispensa 30 na vifaa maalum vya kunawia mikono Mkoa wa Songwe na mikoa yote ya mipakani kama sehemu ya kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu.

Nae, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amesema kuwa, vita dhidi ya ugonjwa huu ni vita inayohitaji ushirikiano na umoja baina ya watu wote katika jamii, huku akiweka wazi kuwa baadhi ya silaha za kupambana dhidi ya ugonjwa huu ni kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka na kuepuka msongamano isiyo na ulazima.

“Tupo katika kipindi ambacho tunahitajiana sana, kila mtu kwa nafasi yake anamuhitaji mwingine, kwahiyo tushirikiane kwa pamoja tunaweza kukabiliana na ugonjwa huu, janga hili haliitaji vifaru, janga hili haliitaji jeshi la anga, janga hili linatuhitaji sisi na utayari wet utu, na nguvu pekee tulionayo ni kunawa mikono, na kuepuka misongamano isiyo yalazima, na utamaduni huu uwe endelevu”, alisema

Uhamasishaji huu unafanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Mkoa wa Songwe, kisha kuelekea Mkoa wa Rukwa.