Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo ameondosha marufuku ya watu kutoka nje ama ‘lockdown’ katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ambayo yalikuwa yamefungwa ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.

Watu sasa wanatakiwa kuvaa barakoa nchini humo, na makatazo kama kufungwa kwa shule na mikusanyiko ya watu bado yangalipo kwa sasa. Mipaka ya nchi hiyo pia itaendelea kufungwa kwa wiki mbili zaidi wakati mapambano dhidi ya virusi vya corona yakiendelea.

Rais Akufo-Addo amesema uauzi huo umekuja baada ya uelewa mzuri wa kasi ya maambukizi na programu kubwa ya kupima watu na kutanua vituo vya kutenga watu pamoja na matibabu.

Mji Mkuu wa Accra, jiji la pili kwa ukubwa Kumasi pamoja na jiji la viwanda Tema yaliwekwa katika marufuku ya watu kutoka nje kwa wiki tatu ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Nchi hiyo mpaka sasa imesharekodi wagonjwa 1,042 wa virusi vya corona na vifo tisa.

Zaidi ya ya sampuli 6,000 zimeshafanyiwa vipimo hivyo nchi Ghana.

Wengi wa waliogundulika na ugonjwa huo nchini humo ni wasafiri ama watu ambao wamekutana na wasafiri.

Serikali ya Ghana pia imeanzisha matumizi ya ndege zisizo na rubani ili kuwahisha utumaji wa sampuli za kufanyiwa vipimo. Nchi hiyo pia imeongeza uzalishaji wa nguo maalumu za wafanyakazi wa afya kujilinda na maambukizi.

Mamlaka pia zimesema zitaendelea kufuatilia kusambaa kwa ugonjwa huo na kuweka marufuku nyengine kama itahitajika katika maeneo yatayokuwa na kasi kubwa ya maambukizi .

 

The post Rais wa Ghana aamuru watu kuanza kutoka nje baada ya Lockdown, Sharti kuvaa Barakoa appeared first on Bongo5.com.