Hali ndani ya uongozi wa Miamba ya soka nchini Hispania klabu ya Barcelona yazidi kuwa mbaya, huku kukionekana kuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe hali iliyopelekea wajumbe sita (6) wa bodi ya Rais wa timu hiyo Josep Maria Bartomeu kuandika barua usiku wa hapo jana siku ya Alhamisi kutangaza kujiuzulu nyazifa zao.

Makamu wa rais, Emili Rousand, Enrique Tombas pamoja na wakurugenzi wa Barcelona, Silvio Elias, Josep Pont, Jordi Calsamiglia na Maria Texidor ndiyo walioamua kuandika barua ya kuachana na Barcelona kipindi hiki ambacho janga la Virusi vya Corona linaendelea kuisumbua Hispania.

Barua ya maamuzi yao imeripotiwa na La Vanguardia na kutafsiriwa katika lugha ya Kiingereza ”Tunapenda kuwasilisha kuwa wakurugenzi waliosaini hapo chini wamemtaarifu Rais Bartomeu juu ya uamuzi wetu wa kujiuzulu nafasi zetu kwenye klabu.”

Sehemu ya barua hiyo iliendelea kwa kusema “Tumefikia hatua hii baada ya kutoona njia ya kubadili vigezo na aina ya usimamizi wa klabu mbele ya changamoto muhimu siku usoni na haswa kutokana na hali mpya ya hili janga (Corona)”.

“Tukiwa katika sehemu ya hatua yetu ya mwisho katika kuihudumia klabu, tunapendekeza kuitishwe kwa uchaguzi mara tu baada ya hali itakapokuwa nzuri ili klabu iweze kusimamiwa katika njia bora zaidi na itakayoweza kushughulikia changamoto zote muhimu kwa siku za usoni,” hayo yakiwa ni sehemu tu ya maelezo ambayo yameandikwa na viongozi hao waliojiuzulu.

Barcelona wanaonekana kuathirika kiuchumi kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona, huku mshambuliaji wao hatari Lionel Messi na wachezaji wengine wakiridhia kukatwa mishahara yao.

Huku klabu hiyo pia ikinukuliwa ikisema kuwa haitagharamikia mishahara ya wafanyakazi, licha ya Bartomeu kusema kuwa timu hiyo ya Barcelona itapata kitita cha paundi milioni 878 msimu huu.

The post Mpasuko watokea ndani ya Barcelona, wajumbe 6 wa bodi wajiuzulu kisa Rais wa klabu na Virusi Corona appeared first on Bongo5.com.