Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forum, Maxece Mello kulipa faini ya Sh.Mil 3 ama kwenda jela mwaka mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kulizuia Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yake.

Pia Mahakama hiyo, imemuachia huru mshitakiwa mwenzake Mickie Mushi baada ya kutotiwa hatiani katika makosa yao.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo upande wa utetezi umedai kuwa utakata rufaa kupinga adhabu hiyo.

Melo yupo chumba cha mahabusu kusubiri kulipa faini hiyo ama akishindwa atumikie kifungo cha mwaka mmoja.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kuzuia Polisi kufanya uchunguzi kinyume na kifungu cha 22 (2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandano namba 14 ya mwaka 2015.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Aprili Mosi, 2016 na Desemba 13, 2016  katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni.