Mbunge wa Konde(CUF) Khatib Said Haji ameiomba Serikali kumchukulia hatua Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Salama Aboud Talib aliyekataa kukaa kwenye karantini na kusababisha maambukizi kwa watu wawili kwenye familia yake.

Akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2020/2021 amesema matokeo ya Hilo nyumbani kwake kuna watu wawili amewaambukiza na huko hospitali haijulikani matokeo yake nini.

“Ndani ya siku tatu ameng’ang’ana kukaa hospitali ya Mnazi Mmoja matokeo yake akatolewa kwa nguvu baada ya kuona jambo hili limekuwa kubwa sana. Baada ya malalamiko makubwa ndio alikubali kuwekwa kwenye karantini,”amesema.

Amesema alifanya hivyo kwa sababu ya kiburi cha madaraka yake na kumpongeza makamu wa pilli wa Rais Zanzibar kwa kukubali kukaa karantini alipotoka nje ya nchi bila kulazimishwa.

“Huu ndio utu, huu ndio ubinadamu leo waziri huyu ni nani anayekataa uamuzi wa Serikali hata uamuzi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.Hatuwezi kumchekea mtu mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu ni waziri ulichukulie hatua haraka."