Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mjiolojia Chone Malembo amesema kuwa kuanzishwa kwa masoko ya madini katika mkoa wa Singida kumeleta mapinduzi makubwa kwenye uchumi ikiwa ni pamoja na makusanyo ya shilingi bilioni 3.243 ambayo ni sawa na asilimia 216.2 kwa mwaka wa fedha 2019-2020 ambao haujamalizika.

Mjiolojia Malembo aliyasema hayo tarehe 17 Aprili, 2020 kwenye ziara ya Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Tume ya Madini na waandishi wa madini katika mkoa huo yenye lengo la kuangazia mafanikio ya Sekta ya Madini katika mkoa wa Singida.

Malembo alifafanua kuwa, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019 – 2020 ofisi yake ilipangiwa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.5 na kuongeza kuwa hadi kufikia katika kipindi cha mwezi Machi mwaka huu, Ofisi yake ilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.243 sawa na asilimia 216.2 na kufanikiwa kupewa cheti cha pongezi kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini .

Alisema siri ya makusanyo ni pamoja na usimamizi mzuri kwenye masoko mawili ya madini yaliyoanzishwa katika maeneo ya Shelui Wilayani Iramba na Manispaa ya Singida mkoani Singida.

Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli kabla ya kuanzishwa kwa masoko husika Malembo alisema kuwa, katika mwaka wa fedha 2018-2019, ofisi yake ilipangiwa lengo la kukusanya shilingi bilioni moja na kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 804.5.

Katika hatua nyingine, Malembo alishukuru kwa ushirikiano aliokuwa akiupata kutoka katika vyombo vya ulinzi na usalama na kuongeza kuwa, ofisi yake imekuwa ikishirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama na Taasisi nyingine za Serikali chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Aliongeza kuwa mafanikio yaliyopatikana ni mazao ya uwepo wa uwazi, uwajibikaji na ushirikiano thabiti wa Serikali kwa ujumla wake na kwa msaada mkubwa wa viongozi wa Wilaya na Halmashauri zote.

Akizungumzia namna ofisi yake inavyodhibiti utoroshaji wa madini alisema kuwa mkoa umeanzisha Kikosi Kazi Madini (KKM) ambacho kina wajumbe kutoka taasisi muhimu ikiwemo baadhi ya taasisi zinazounda kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

Alisisitiza kuwa kikosi kazi hukutana mara kwa mara ili kupitia taarifa na kujadili na kisha kutengeneza mikakati madhubuti inayosaidia udhibiti wa utoroshaji wa madini na ukwepaji wa kulipa tozo za Serikali.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iramba Emmanuel Luhahula akielezea mchango wa sekta ya madini katika wilaya yake, mbali na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa usimamizi mzuri wa sekta ya madini ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini nchini, alisema mapato katika halmashauri ya Iramba yameongezeka hadi shilingi milioni 99 tofauti na awali ambapo walikuwa wakipata shilingi 500,000 kwa mwaka.

Aliongeza kuwa, uanzishwaji wa masoko ya madini umepunguza kwa kiasi kikubwa cha utoroshaji wa madini kwa kuwa wachimbaji wa madini wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuyatumia masoko ya madini yaliyoanzishwa na kupata faida huku Serikali ikipata kodi mbalimbali.

Luhahula alitaja mafanikio mengine ya masoko ya madini yaliyoanzishwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha katika wilaya ya Iramba na kuwataka wachimbaji kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kanuni za madini huku wakijikinga na ugonjwa wa korona.

Akielezea mikakati ya wilaya yake kwenye udhibiti wa ugonjwa wa korona hususan kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini Lahahula alisema, Ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida wameshaanza kutoa elimu kwa wachimbaji wa madini na kuhakikisha wachimbaji wanaendesha shughuli zao kwa tahadhari ikiwa ni pamoja na kuwa na maji tiririka na vitakasa mikono.

Wakati huohuo wakizungumza kwa nyakati mbalimbali wachimbaji wa madini katika machimbo ya dhahabu ya Sekenke mbali na kuipongeza Serikali kwa kuwapatia maeneo ya uchimbaji wa madini na uanzishwaji wa masoko ya madini walisema kuwa masoko ya madini yameleta mapinduzi makubwa.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wa madini, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wachimbaji Wadogo wa Madini Kisonga na Shelui (UWAWAKISHE), Masumbuko Jumanne alisema kuwa kuanzishwa kwa masoko ya madini kumeleta manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kuuza madini yao kwa kufuata bei elekezi zinazotolewa na Serikali kila mwezi na kupata faida na usalama kwenye biashara ya madini.