Marekani imeendelea kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na corona Duniani ambapo hadi muda huu wamefariki Watu 52,217.

Marekani pia inaongoza  kwa visa, vimefikia 925,758  na wamepona 110,432.

Wakati huo huo Ofisi ya Bajeti ya Congress ya Marekani imetoa ripoti ikionyesha kuongezeka kwa asilimia 14 ya ukosefu wa kazi nchini humo.

Ofisi hiyo imesema kwamba ongezeko hilo la uhaba wa ajira limeripotiwa katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu wa 2020.

Hii ni katika hali ambayo mamilioni ya Wamarekani wamepoteza ajira  au wanakadiriwa kupoteza nafasi hizo za kazi katika miezi michache ijayo.

Alhamisi iliyopita, Wizara ya Kazi ya Marekani ilitoa ripoti yake ya kila wiki ikisema kuwa tayari watu milioni 26 wamepoteza nafasi zao za kazi katika kipindi cha wiki tano zilizopita kutokana na kuenea kwa kasi nchini humo virusi hatari vya corona.


Kuenea virusi hivyo katika pembe zote za nchi hiyo kumepelekea viwanda na vituo vingine vya uzalishaji ajira kufungwa na hivyo kuifanya nchi hiyo ikabiliwe na mgogoro mkubwa wa kiuchumi.