Rais wa Marekani Donald Trump ameagiza serikali yake kusitisha kutoa fedha kulifadhili Shirika la Afya Duniani WHO, kwa kile anachosema Shirika hilo limeshindwa kudhibiti mambukizi ya virusi Corona.

Hatua hii ya rais Trump imekuja baada ya rais huyo wa Marekani kulishtumu WHO kwa kuegemea upande wa China katika vita dhidi ya maambukizi haya.

“Uongozi wangu utasitisha ufadhili kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) wakati Shirika hili likiwa linachunguzwa katika majukumu yake yaliyoshindwa kutimizwa katika kukabiliana na usambaaji wa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, “ amesema Rais wa Marekani Donald Trump.

Wakati huo huo rais Trump ameushutumu Umoja wa mataifa kwa kutoweza kukabiliana na kusambaa kwa janga la Covid-19 ambalo lilianzia nchini China, na 'linapaswa kulaumiwa'.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa “huu si wakati wa kukata ufadhili kwa WHO”.

Hayo yanajiri wakati shirika la afya duniani limesema kuwa visa vya maambukizi ya virusi vya Corona vinapungua nchini Italia na Uhispania tofauti na Uingereza, Uturuki na Marekani ambapo visa vya maambukizi vinazidi kuongezeka.

Hata hivyo msemaji wa WHO, daktari Margaret Harris amesema asilimia 90 ya visa vipya vya maambukizi ya virusi vya Corona kwa sasa hivi vinatokea Ulaya na Marekani na wala sio China, ambayo ilikuwa kitovu cha maambukizi ya virusi hivyo.