Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya mvua kubwa kwa siku mbili kuanzia kesho katika mikoa 15 ikiwamo Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo, katika siku hizo, kutakuwa na mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya na Rukwa.

Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri wa Hali ya Hewa (TMA), Samuel Mbuya, alisema kutokana na tahadhari hiyo, athari zinazoweza kutokea kwenye maeneo hayo ni makazi na barabara mbovu kuzungukwa na maji hali itakayosababisha kukosekana kwa makazi na adha ya usafiri.

Kwa siku ya Ijumaa, alisema mvua kubwa inatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, Zanzibar, Pwani, Mafia, Tanga, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro na kujirudia tena mikoa ya Njombe na Iringa.

Mbuya alisema kutokana na tahadhari hiyo, wakazi wa mikoa hiyo wanapaswa kuchukua hatua za kujikinga na kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na TMA.