Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amefikia makubaliano ya kihistoria ya kuunda serikali ya pamoja ya dharura na hasimu wake mkuu Benny Gantz, hatua inayomaliza mkwamo mbaya kabisa wa kisiasa nchini humo.

Bildkombo Israel Gantz Netanjahu (Reuters/C. Kern/A. Cohen)

Makubaliano hayo ya miaka mitatu yatamruhusu Netanyahu kubakia mamlakani kwa muda wa miezi 18 katika kipindi ambacho anatarajiwa kupandishwa kizimbani kujibu mashtaka ya rushwa yanayomkabili.

Baada ya muda huo, hasimu wake Gantz mwenye umri wa miaka 60 ambaye sasa ni spika wa bunge atachukua wadhifa wa waziri mkuu kwa muda wa miezi 18 mingine kabla ya kutiishwa duru mpya ya uchaguzi nchini Israel.

Licha ya Netanyahu kupata ushindi mdogo dhidi ya Gantz katika duru tatu za uchaguzi mwaka uliopita, wanasiasa hao wote wawili hawakufanikiwa kuwa na wingi wa viti bungeni kuweza kuunda serikali.

Kufuatia kuzuka kwa janga la viruis vya corona, wito wa kuunda serikali ya pamoja uliongezeka nchini Israel kwa lengo la kuweka mikakati ya kudhibiti kuenea mzozo huo wa kiafya.

Netanyahu na Gantz wasifu makubaliano yaliyofikiwa 

Israel | Massen-Demo gegen Netanjahu trotz Corona-Verbot (Getty Images/AFP/J. Guez)

Kufuatia kufikiwa makabaliano hayo Netanyahu aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa ametimiza ahadi  ya kuipatia Israel serikali ya pamoja itakayofanya kazi ya kulinda maisha ya raia wa nchi hiyo.

Kwa upande wake Gantz aliandika kupitia Facebook kuwa mkataba uliofikiwa umezuia kufanyika duru ya nne ya uchaguzi.

Kuhusu makubaliano hayo mkaazi mmoja wa mjini Tel Aviv Avi Alka Llay amesema “Nadhani ni suluhisho bora kwa sababu sasa tuna zaidi ya watu milioni moja wasio na ajira na biashara nyingi sasa zipo kwenye hali ya mkwamo, kwa hivyo tunahitaji kuwa na serikali katika kipindi hiki.”

Chini ya makubaliano yaliyofikiwa nafasi katika baraza la mawaziri zitagawanywa kwa usawa kati ya chama cha Likud cha Netanyahu na kile cha mrengo wa kushoto cha Buluu na Nyeupe kinachoongozwa na Gantz.

Pindi serikali mpya itaundwa, Gantz atatambuliwa rasmi kuwa waziri mkuu mteule na atapaswa kuwachia wadhifa wa spika akisubiri muda wa miezi 18 kuwa waziri mkuu kamili.

Palestina ina wasiwasi na serikali mpya itakayoundwa 

Israel: Wohnungsbau in Ostjerusalem (picture-alliance/N. Alon)

Moja ya suala muhimu wakati wa mazungumzo ya kuunda serikali hiyo ilikuwa ni utekelezaji wa mpango tata wa rais Donald Trump wa Marekani kuhusu Mashariki ya Kati ambao utaipatia Israel ruhusu ya kuyachukua kwa nguvu maeneo zaidi kwenye eneo la ukingo wa magharibi.

Sehemu ya makubaliano kati ya Gantz na Netanyahu yatamruhusu waziri mkuu wa Israel kutekeleza mapendekezo ya mapngo wa Trump.

Mpango huo wa rais trump umekabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka jumuiya ya kimataifa na wapalestina.

Waziri mkuu wa Palestina Mohammad Shtayyeh amesema kuundwa kwa serikali hiyo ya Israel kunahitimisha ndoto ya kuwa na suluhisho la mataifa mawili katika mzozo wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina.

The post Makubaliano ya kuunda serikali yafikiwa Israel appeared first on Bongo5.com.