Watu 7 wanaotuhumiwa kuwa majambazi, wameauawa katika eneo la Kata ya Kumwambu, Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma baada ya kukabiliana na Polisi wakati wakijiandaa kufanya uvamizi na kupora katika kampuni ya ujenzi wa barabara ya Sino Hydro Engineering Company Ltd.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, ACP Martin Otieno, alisema tukio hilo limetokea juzi saa tano usiku baada ya jeshi hilo kupokea taarifa ya kikundi kinachopanga kwenda kutekeleza uhalifu huo.

Kamanda Otieno alisema kufuatia taarifa hizo, kikosi kazi kilijipanga kwenda kuimarisha ulinzi katika maeneo ambayo walipanga kujificha na baadaye kuona kundi la watu 12 wakitembea kuelekea kutimiza adhima yao na walipobaini kuwa wanafuatiliwa walianza kuwarushia risasi askari na kuibuka majibizano ya risasi yaliyodumu kwa takribani dakika 25.

Pia, Kamanda Otieno alisema katika majibizano hayo askari waliwaua majambazi watatu hapo hapo na wanne walikufa njiani wakati wakipelekwa hospitali ya wilaya ya Kibondo huku wengine watano wakikimbia kusikojulikana.

Jeshi hilo pia limekamata bunduki tatu zilizotengenezwa kienyeji, pisto moja, risasi 89 za SMG, 15 za pisto na kofia za kuficha sura ambazo zilikuwa zikitumika katika uhalifu.