Serikali ya Korea Kusini inaangalia undani wa taarifa zilizoripotiwa na Vyombo vya Habari vya Marekani kuwa Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ana hali mbaya baada ya kufanyiwa upasuaji.

Maafisa wa Korea Kusini wamesema hawawezi kudhibitisha ripoti hiyo mara moja. 

CNN kimemnukuu Afisa wa Marekani ambaye alisema Kim yupo katika hali mbaya baada ya kufanya upasuaji ambao haukuwekwa wazi.

Kumekuwa na sintofahamu kuhusu afya ya Kim baada ya Kiongozi huyo kushindwa kuhudhuria hafla ya Kumbukumbu ya Marehemu babu yake, Kim Il Sun ambaye pia ni muasisi wa Taifa hilo wiki iliyopita.

Inaelezwa kuwa afya ya Kim Jong Un imezorota miezi ya hivi karibuni kutokana na uvutaji sigara, unene uliopitiliza na kufanya kazi kwa muda mrefu.

Alionekana kwa mara ya mwisho Aprili 11 ambapo aliongoza kikao na kisha kuelekea hospitali, chanzo kimoja kimesema kuwa Kim amekuwa akiugua tangu Agosti mwaka jana.