Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza habari ya kuthibitishwa kesi nyingine moja ya ugonjwa wa Ebola huko Jamhhuri ya Kidemokrasia ya Congo zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya kutangazwa rasmi kumalizika kabisa ugonjwa huo nchini humo.

Dk Tedros Adhanom, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema kuwa, licha ya kwamba katika kipindi cha siku 52 zilizopita hakuna hata kesi moja ya ebola iliyoripotiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lakini jana Ijumaa kuna kesi moja imethibitishwa kuwa ni ya ugonjwa huo.

Tangazo la kugunduliwa kesi hiyo mpya limekuja zikiwa zimebakia siku chache tu kabla ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutangaza kumalizika kabisa ugonjwa huo nchini humo.

Wimbi jipya la maambukizi ya ebola lilianza tarehe 8 Mei 2018 katika mji wa Bikoro wa mkoa wa Ikweta wa kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na baadaye ulienea katika makao makuu ya mkoa huko yaani mji wa Mbandaka kabla ya kufika katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilikuwa inajiandaa kutangaza kumalizika kabisa ugonjwa huo siku ya Jumatatu, lakini Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, anasikitika kusema kuwa nchi hiyo haiwezi tena kutangaza kumalizika ugonjwa huo siku ya Jumatatu.

Mbali na ugonjwa wa Ebola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekumbwa pia na maambukizi ya corona na hadi hivi sasa watu 215 wamethibitishwa kukumbwa na ugonjwa huo nchini humo huku 20 kati yao wakiwa wameshafariki dunia.