SALVATORY NTANDU
Katika jitihada za kukabiliana na Maambukizi ya  Ugonjwa uanaosababishwa na virusi vya Corona mkoani Shinyanga, Kampuni ya uchimbaji madini ya Dhahabu ya Barrick Buzwagi imekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Shilingi  Milioni 48 kwa mkuu wa mkoa huo Bi Zainab Tellack ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya virusi hatari vya COVID 19.

Akikabidhi vifaa hivyo Aprili 18 mwaka huu,wilayani Kahama kwa Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi Zainab Tellack niaba ya Kampuni ya Barrick Buzwagi Mkuu wa Kitengo cha Usalama na Afya Kazini Mgodi wa Barrick Buzwagi, Dk. Antoinette George amesema kuwa  msaada huo umejumuisha makontena 25 ya kunawia mikono kwa mkoa wa Shinyanga na 30 kwa wilaya ya Kahama, Chroline ndoo tano zenye kilogramu 45 kila moja, gloves pea 50 zitakazotumika kwa watoa huduma, Barakoa (mask) 400, Chemical Suits 40, chemical googles 40 na vipimia joto saba.

Amefafanua kuwa vifaa hivyo  vitatumika katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi mkoani humo  hususani katika  Masoko, Minada, Vituo vya Mabasi, Magerezani, pamoja na  Vituo vya Afya ili kuwakinga wananchi dhidi ya janga la kidunia la Ugonjwa  COVID 19.

“Sisi kama Barrick tumetoa   magari manne ya kutoa elimu juu ya ugonjwa huu hatari wa COVID 19 ambayo yatatoa  matangazo  katika maeneo mbalimbali mkoani Shinyanga kwa muda wa miezi miwili sambamba na  kutoa mafunzo kwa maofisa afya 204 kwenye vijiji vyote wilayani Kahama”, alisema Dk George..

Awali  akipokea vifaa hivyo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Bi  Zainab Telack ameishukuru Kampuni ya Barrick Buzwagi kwa msaada huo ambao utasaidia kuongeza nguvu katika mapambano dhindi ya Ugonjwa huu na kuwataka wananchi pindi vifaa hivyo vitakapowekwa kwaajili ya matumizi ni budi wananchi wakazingatia maelekezo ya Serikali ili kujikinga  na COVID 19. 

Mbali na hilo Bi  Tellack ametoa onyo kali kwa wananchi mkoani humo kuacha kutoa taarifa za uongo kuhusiana na ugonjwa huo huku akitolea mfano tukio la kukamatwa kwa mkazi  Mwakitolyo , Mussa Kisinza aliyempigia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akimdanganya kuwa  anaugonjwa wa COVID 19

"Serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wotw watakaobainika kusambaza taarifa uongo kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na ugonjwa huu tutahakikisha tunawashughulikia wote wanaoleta mizaha tunahitaji wananchi wetu wabaki salama na janga hili”,alisema Tellack.

Kwa upande wake  Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha alisema kuwa  katika wilaya ya kahama kuna  mwingiliano mkubwa wa watu na uwepo wa mabasi mengi ya abiria yanayoanzia safari zake mjini hapo kuelekea mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Bukoba, Arusha na Kilimanjaro na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa COVID 19.

Amefafanua kuwa   wameendelea kuchukua tahadhari katika maeneo yote yenye mikusanyiko na wananchi wameonyesha mwitikio kwa kuunga mkono jitihada hizo za serikali isipokuwa bado changamoto ipo kwa waendesha pikipiki (bodaboda) na wamiliki wa Baa ambao hawataki kufuata maelekezo ya serikali.

Mwisho.