Mkurugenzi mkuu wa Shirila la Fedha Duniani IMF Bibi Kristalina Georgieva amesema kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona, uchumi wa dunia kwa mwaka huu unakadiriwa kushuhudia mporomoko mkubwa zaidi tangu miaka ya 30 ya karne iliyopita.

Amesema mlipuko wa virusi vya Corona ni msukosuko pekee, ambao unavuruga kwa kasi na kwa kina utaratibu wa kijamii na kiuchumi kote duniani. 

Katika miezi mitatu iliyopita, IMF ilikadiria kuwa mapato ya watu katika nchi wanachama zaidi ya 160 yataongezeka mwaka huu, lakini kwa sasa shirika lake limekadiria kuwa mapato hayo katika nchi zaidi ya 170 yatapungua mwaka huu. 

Shirika hilo litatoa ripoti mpya kuhusu makadirio ya ukuaji wa uchumi wa dunia wiki ijayo.

Ameongeza kuwa kama mlipuko wa virusi vya Corona utadhibitiwa katika nusu ya pili ya mwaka huu, na nchi zote zitarejesha shughuli za kiuchumi, uchumi wa dunia utafufuka kwenye baadhi ya sehemu, lakini bado utakabiliwa na sintofahamu kubwa.