Mfanyabiashara Said Nasser Nassor {Bopar} Kushoto
akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Mashine za Kupimia Joto kukamilisha ahadi aliyotoa Wiki iliyopita ya mchango wake wa kusaidia Vifaa kwenye mapambano dhidi ya Virusi vya Corona.
 Balozi Seif akiangalia moja ya Mashine hiyo ya kupimia Joto
la mwili inayosaidia kutoa viashiria vya kutambua matatizo ya maradhi kwenye Mwili wa Mwanaadamu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akitoa shukrani mara baada ya kupokea Mchango wa Mashine na Mashuka kutoka kwa Mfanyabiashara Said Bopar Ofisini kwake Vuga Mjini anzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
                                                   Press Release:-
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametahadharisha kwamba wakati umefika sasa kwa kila Mwanajamii kujenga Utamaduni wa kuvaa Kibarkoa katika harakati zake za Kimaisha ili kujiepusha maambukizi ya Virusi vya Corona.
Alisema Taifa bado liko katika kipindi kigumu kutokana na wimbi la Maambukizo ya Virusi hivyo ambavyo hivi sasa vinazunguuka ndani ya Mitaa baada ya Serikali kufanikiwa kuzuia maambukizi kutoka Nje ya Nchi kwa kufuta muingiliano wa safari za Kimataifa .
Balozi Seif Ali Iddi alitoa tahadhari hiyo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar mara baada ya kupokea msaada wa Mashuka 20 na Mashine 30 za kupimia joto la mwili zilizotolewa na Mfanyabiashara Maarufu Nchini Nd. Said Nasser Nassor {Bopar} akikamilisha msaada aliyoahidi kutoa katika kuungana na Serikali Kuu kwenye mapambano dhidi ya kuenea kwa Virusi vya Corona Nchini.
Balozi Seif alisema Ugonjwa wa Mafua na Homa kali ya mapafu inayosababishwa kupumua kwa shida pamoja na kikohozi kutokana na Virusi hatari vya Corona umo ndani ya jamii ukisambaa jambo ambalo linahitaji kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa.
Alisema katika vita hivyo vigumu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inahamasisha Viwanda Vidogo Vidogo Nchini kutengeneza vibarkoa ili kuwapunguzia gharama kubwa Wananchi hasa wale wa kipato cha chini wanaolazimika kununua vifaa hivyo kutoka Nje ya Nchi kwa bei ya juu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza na kumshukuru Mfanyabiashara Said Nasser Nassor {Bopar} kwa Uzalendo wake anaojitolea wa kusaidia Jamii pale inapopata changamoto na mitihani tofauti.
Balozi Seif  alibainisha wazi kwamba msaada huo wa mashuka na Mashine za kupimia joto la Mwili zinazoashiria kuelewa kuutambua Ugonjwa mapema ni muhimu na kwa upande mwengine zitasaidia nguvu ya Serikali katika jitihada zake za kupambana na maradhi yanayowasumbua Wananchi.
Aliwakumbusha Wananchi kutoona shinda kuendelea kutumia Dawa za asili kama vile nyungu na vyakula vyenye asili ya ukali {Vitamin C} ambavyo kwa mujibu wa Wataalamu wa Afya ni rahisi kusaidia kupambana na Virusi Thakili vya Corona.
Mapema akikabidhi mashuka na Mashine hizo za kupimia Joto la Mwili kukamilisha ahadi yake Mfanyabiashara Said Nasser Nassor { Bopar } ameendelea kusisitiza kwamba yuko tayari Siku na muda wowote kusaidia Jamii na Serikali pale linapotokea suala la dharura inayoikumba Jamii.
Said Bopar alisema yeye kama Mzalendo na Mwananchi wa Taifa hili hana sababu ya kutoiunga mkono Serikali Kuu pale inapotokea dharura au kuombwa kufanya hivyo kwa maslahi ya Taifa na Wananchi wake wote.
Wiki iliyopita Mfanyabiashara huyo tayari ameshakabidhi msaada wa Vitanda, Sabuni, Vitakasa Mikono, Dawa ya Mbu, Magodoro, Mito, Tishu na Mashuka kwa ajili ya kuhudumia Mapambano dhidi ya kuangamiza Virusi vya Corona hapa Nchini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
27/04/2020.