Na Amiri kilagalila,Njombe
Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri amewaagiza maafisa tarafa kuwafungia biashara wafanyabiashara watakaobainika wamepandisha bei vitakasa mikono zikiwemo ndoo za maji katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya COVID-19.

Ametoa agizo hilo hii jana katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Njombe kilichofanyika nje ya ofisi ya wilaya ya Njombe wakati wakipokea taarifa rasmi za kamati za utekelezaji wa mapambano dhidi ya maambukizi ya Corona  (COVID -19) wilayani humo.

“Kwa hiyo maafisa tarafa watu wa namna hiyo huko vijijini kwenu awe ni mjini tafadhari ita afisa biashara weka kufuli halafu hatua nyingine zitachukuliwa hapo baadaye”

Aidha amesema kwa mujibu wa maelekezo ya serikali kwa wafanyabiashara wa namna hiyo kwa kipindi ni kumfungia biashara.

“Wako baadhi ya wafanyabiashara ambao kwasababu zao wenyewe wamepandisha bei za vifaa hivi hasa ndoo kwa ajili ya kusafisha mikono,sasa maelekezo tuliyopewa kama kuna mfanyabiashara yeyote anaamua kupandisha bei za vifaa hivi ambavyo vinahitajika sana kwa kipindi hiki ni kumfungia biashara yake ndicho tulichoelekezwa,kwa hiyo maafisa tarafa ukiona kweli mtu amepandisha bei ya ndoo,koki,amepandisha bei ya sabauni za mikono nipe taarifa kinachofuata tunamfungia biashara,hayo tukiyatekeleza vizuri hakuna yeyote atakayekwenda kinyume”alisema tena Ruth Msafiri

Ruth Msafiri ametoa agizo kabla ya kuhitimisha kikao cha kamati ya ulinzi na usalama mara baada ya kupokea taarifa ya afisa tarafa wa tarafa ya Njombe mjini Lilian Nyemele kukutana na changamoto hiyo kwa wafanyabiashara.

“Imejitokeza changamoto kwa baadhi ya wafanyabiashara kuuza ndoo hizi za maji kwa ghalama,awali ndoo ya lita kumi iliuzwa kwa shilingi elfu 7 na sasa kufikia shilingi elfu kumi,na ndoo kubwa iliuzwa elfu 12 na sasa imefika elfu 18 lakini tumefanya jitihada na kutoa maelekezo kwamba kupitia ugonjwa huu sio fursa ya kujinufaisha”alisema Lilian Nyemele.

Vile vile katika muendelezo wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na kirusi cha COVID- 19,mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri na wataalamu wa afya mbele ya kamati ya ulinzi na usalama amezindua kipeperushi maalumu chenye maelekezo muhimu juu ya ugonjwa huo pamoja na mashine ya kutakasa mikono pasina kugusa na mikono.

Isdory Kiyenze ni meneja wa shirika la viwanda vidogo vidogo sido mkoa wa Njombe ambaye amesema wao wamelazimika kutengeneza mashine maalumu ya kunawia mikono bila kugusa sehemu yoyote zaidi ya kukanyaga pedali unapohitaji kutoa maji au sabuni wakati wa kunawa mikono, ambayo itakuwa rahisi kwa ajili ya kuepusha madhara zaidi ambayo itasambazwa kwenye taasisi mbalimbali za umma huku wakipanga kutengeneza na ndogo ambazo zinaweza kutumika hata kwenye ngazi ya familia.