Wakati wanasayansi wakichuana kutafuta kinga ya ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19, serikali ya China imeruhusu majaribio mawili zaidi ya chanjo ya kudhibiti ugonjwa huo uliogeuka janga duniani.

Jumatatu, mamlaka ya serikali ya chakula na dawa, iliidhinisha chanjo moja iliyotengenezwa na kampuni ya Sinovac Biotech ambayo imesajiliwa katika soko la Nasdaq na makao yake makuu ni Beijing, alisema Wu.

Aliongeza kuwa chanjo nyingine inayotengenezwa na Taasisi ya Bidhaa za Kibaiolojia ya Wuhan pamoja na Taasisi ya Virolojia ya Wuhan, iliidhinishwa Jumapili.

Ingawa habari hizo zinatia matumaini, Dk Tumaini Haonga aliiambia Mwananchi kuwa bado mchakato utachukua muda kabla ya chanjo hiyo kuanza kutumika.

“Chanjo ikitengenezwa maabara na kujiridhisha, unatakiwa uanze kuijaribu kwa viumbe hai ili kuangalia kama ina madhara ya kiafya. Kama inaleta faida na kukinga kweli unatakiwa ujaribu kwa watu walio hatarini kuambukizwa,” alisema Dk Haonga.

“Majaribio hayafanyiki eneo moja. Ni lazima iwe maeneo tofauti kwa watu wenye asili, umri na jinsia tofauti ili kuweza kujiridhisha na matokeo. Kwa kawaida majaribio ya chanjo huchukua hadi miezi 18 kuthibitishwa lakini zipo zinazochukua muda zaidi.”

Maoni kama hayo alikuwa nayo Dk Timizael Sumuni wa Hospitali ya TPC mjini Moshi. “Kinachofanya mchakato wa kutengeneza chanjo katika mazingira ya kawaida kuwa mrefu ni uangalifu na umakini unaosababishwa na kuhakiki usalama wa chanjo husika,” alisema.

“Pia kufuatilia madhara ya muda mfupi, wa kati na muda mrefu yanayoweza kujitokeza kutokana na chanjo yenyewe.”

Lakini aliona haja ya kutofuata taratibu za kawaida kutokana na athari za virusi hivyo vipya.

“Kwa mwenendo na hatari ya ugonjwa huu wa Covid-19 inalazimu kukiuka taratibu nyingi kwa kuwa mlipuko huu hausubiri, unaendelea kuua watu, hususan wenye umri mkubwa,” alisema.

“Madhara ya kuharakisha mchakato ni madogo kuliko yale ya kufuata utaratibu wa kawaida. Binafsi naona ni jambo jema kabisa kuondokana na taratibu za kawaida katika kushughulikia upatikanaji wa chanjo hii wakati huu wa shaka kubwa.”

Lakini akiongea na Al Jazeera, John Nicholls, profesa wa tiba katika Chuo Kikuu cha Hong Kong, alisema: “Chanjo haitakiwi iharakishwe”.

Timu yake ilikuwa ya kwanza nje ya China kuzalisha virusi maabara kwa ajili ya utafiti.

“Kwa kawaida unaanza chanjo na wanyama wadogo baadaye kwa wakubwa na baadaye kwa binadamu, kitu ambacho huwa ni uamuzi wa kijasiri,” alisema.

“Vifo vingi katika ugonjwa huu ni katika umri mkubwa, kwa hiyo kitu bora ingekuwa ni kuangalia kingamwili zinapokeaje kwa wazee kuliko kwa vijana.”

China iliidhinisha majaribio ya kwanza kwa chanjo iliyotengenezwa na Kituo cha Sayansi ya Tiba cha Kijeshi pamoja na kampuni ya CanSino Bio ya Hong Kong Machi 16.

Source: Mwananchi

The post China yapitisha majaribio ya chacho mbili za corona, mchakato wa muda mrefu kuepukwa appeared first on Bongo5.com.