SALVATORY NTANDU
Mkazi wa mtaa wa Nyasubi ambaye ni mwendesha bodaboda wilayani Kahama mkoani shinyanga, Tumaini Julius (28) amefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya kahama kwa tuhuma ya kubaka mwanafunzi (16) kidato cha tatu katika shule ya sekondari Kishimba.

Akisoma shauri hilo la Jinai namba 115/2020 Aprili 15 mwaka huu Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Shabani Mateso mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidi wa Mahakama hiyo Evodia Kyaruzi alidai kuwa Tumaini alitenda kosa hilo April 9 mwaka huu katika eneo la Nyasubi.

Mateso alifafanua kuwa Mtuhumiwa alimtorosha mwanafunzi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa na kuishi nae  kama mke na Mume tangu Aprili 3 hadi 9 alipokamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi Kahama.

"Tumaini ambaye ni mwendesha bodaboda alimshawishi mwanafunzi huyo baada ya kukutana nae nyakati za usiku akiwa anatokea kwa rafiki yake Bukondamoyo baada ya kuogopa kurudi nyumbani kwa wazazi wake ambao ni wakali ndipo akamhadaa atampeleka bure na  kuanza kuanza kuishi nae Kama mke na mume", alisema Mateso.

Mateso alisema kuwa  Tumaini alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 130 (1)(2)(e) na 131(1)cha kanuni ya sura 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka  2019.

Tumain amekana Shitaka hilo na Shauri hilo limeahirishwa hadi Aprili 28 mwaka huu na amepelekwa rumande baaada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Mwisho.