Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
AZIMIO namba 64/292 la mwaka 2010 la Umoja wa Mataifa linatamka kuwa huduma ya maji na usafi wa mazingira ni haki ya msingi ya binadamu na pia ni hitaji muhimu kwa maisha ya viumbe hai na shughuli mbalimbali za kiuchumi. 


Uwepo wa rasilimali za maji za  kutosha, miundombinu ya usambazaji maji na usafi wa mazingira, na uwezo wa kiuchumi wa kuwekeza na kuendesha huduma za maji ni masuala ya msingi na muhimu katika kufikia lengo hilo.

Katika kutekeleza Sera ya 9 Maji ya Taifa ya mwaka 2002, Wizara ya Maji ina jukumu la kuhakiki ubora na usalama wa maji katika vyanzo vya maji na mitandao ya kusambaza maji kwa lengo la kulinda afya za wananchi na mazingira.

Hali ya huduma ya maji nchini huangaliwa kwa kuzingatia miundombinu ya maji iliyopo na idadi ya watu wanaopata huduma ya maji, ambapo kwa maeneo ya mijini, kiwango hicho hukokotolewa kwa kuangalia idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mtandao wa maji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira.

Huduma ya maji katika maeneo ya mijini hutolewa na Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Miji Mikuu ya Mikoa, Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na maeneo yanayohudumiwa na Miradi ya Kitaifa. 

Mamlaka hizo zimeendelea kutekeleza miradi ya maji kwa kujenga, kukarabati na kufanya upanuzi wa miundombinu ya majisafi katika maeneo ya miji hiyo, ambapo malengo ya Serikali ni kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Miji Mikuu ya Mikoa kufikia asilimia 95 na Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa kufikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2020. 

Malengo ya Serikali ni kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Miji Mikuu ya Mikoa kufikia asilimia 95; na Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa kufikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2020. Kwa upande wa huduma ya uondoaji wa majitaka, lengo la Serikali ni kuongeza huduma hiyo kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2020.

Hadi mwezi Aprili 2019, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo yanayohudumiwa na Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Miji Mikuu ya Mikoa ni asilimia 80 na kwa Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa upatikanaji wa huduma hiyo ni asilimia 64.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Lindi (LUWASA) inatekeleza Mpango wa Uboreshaji wa Huduma ya Maji katika Mji wa Lindi (Mradi wa Maji Ng’apa) unaolenga kutoa huduma ya majisafi kwa wakazi wote waishio eneo la Manispaa ya Lindi na kuondoa changamoto iliyopo ya wananchi hao hulazimika kufuata  maji umbali mrefu kupitia Virula(Vioski).

Akizungumza katika mahojiano maalum na Maafisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO) waliofanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali Mkoani Lindi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Lindi (LUWASA), Mhandisi Juma Sudi anasema anasema mradi huo umekamilika kwa asilimia 92 na hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji wa Lindi ni asilimia 75 kwa sasa. 

Mhandisi Sudi anasema mradi huo ulioanza miaka miwili ulioanza mwaka 2013 na kutarajiwa kukamilika mwaka 2015, una jumla ya visima saba vinavyozalisha maji wastani wa mita za ujazo 7500 kwa siku, huku mahitaji halisi ya huduma ya maji katika Manispaa ya Lindi ni wastani wa mita za ujazo 5000.

Alisema mwezi Februari mwaka huu, Serikali ilitoa kiasi cha Tsh. Bilioni 32 kwa ajili ya kukamilisha hatua mbalimbali zilizosalia katika mradi wa maji wa Ng’apa na mkandarasi mpya wa mradi huo kampuni ya Shanx Corporation Company Ltd Ltd tayari ameanza kazi hiyo ambayo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Julai mwaka huu.

‘’Serikali imeweka fedha nyingi sana katika mradi huu,ni uwekezaji mkubwa unaleta maji katika maeneo yote ya Mji, tunamshukuru sana Rais Dkt, John Magufuli kwa kutoa fedha hizi amefanya maamuzi magumu, sisi LUWASA tumejipanga kuhakikisha tunapeleka huduma ya maji katika maeneo yote ya mjini’’ alisema Mhandisi Sudi.

Aidha Mhandisi Sudi anasema kuwa katika kuhakikisha kuwa tatizo la huduma ya maji katika Mji wa Lindi linatatuliwa kwa haraka, Serikali kupitia Wizara ya Maji imetoa kiasi cha Tsh Bilioni 2.9 kwa ajili ya kujenga mtandao wa mabomba katika Mji wa Lindi ili kuhakikisha kuwa wakazi wote wanapata huduma ya maji wakiwa majumbani kwao.

‘’Mwanzo kabisa wananchi wa Manispaa ya Lindi walikuwa wakipata huduma ya maji kutoka katika chanzo cha kitunda ambacho kipo ng’ambo ya bahari ambao ulikuwa ukizalisha wastani wa mita za ujazo 2000 kwa siku na hata hivyo hakuweza kukidhi mahitaji, hivyo kukamilika kwa mradi huu wa Ng’apa utakuwa mkombozi kwa wananchi wa Manispaa ya Lindi’’ alisema Mhandisi Sudi.

Anaongeza kuwa moja ya kazi inayofanywa na mkandarasi mpya kwa sasa ni pamoja na kuhakikisha anakamilisha kuweka mfumo katika mtambo ili kusukuma maji katika visima vyote vilivyopo umbali wa kilometa 13 kutoka katika chanzo cha Ng’apa pamoja na kukamilisha kazi ndogondogo zilizosalia katika mradi huo.

Kwa upande wake Bi Amina Ally Mkazi wa Kilimahewa Manispaa ya Lindi, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwani kwa sasa wameokoka na matatizo ya ukosefu wa huduma ya maji katika maeneo yao kwani hapo awali walikuwa wakitembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta maji.

‘’Tunaishukuru Serikali kwani imetutua ndoo kichwani sisi akina Mama, kwa sasa Maji yanapatikana katika maeneo yetu hatufuatani tena na akina Baba kwa ajili ya kutupeleka kuchota maji, ambayo yaliyokuwa yakipatikana maeneo ya porini, ambako kulikuwa na vitisho mbalimbali kwa sisi akina mama’’ anasema Amina.

Anaongeza kuwa kwa sasa afya zao zimeimarika kwani hawabebi mizigo mizito kichwani ya ndoo walizokuwa wakisafiri nazo kwa umbali mrefu, kwani Serikali imerahisisha kwa kiasi kikubwa kwa kufunga mtandao wa mabomba ambayo yamerahisisha huduma ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Kilimahewa, ambao jiografia yakekwa kiasi imetawaliwa na milima mingi.

Aidha anasema kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika eneo lao imekuwa nzuri kwani virula (vioski) vilivyofungwa katika sehemu ya eneo la Kilimahewa vipo karibu na makazi ya wananchi na maji hayo ni safi na salama kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani.

Naye Bi. Zubeda Hamadi, Mkazi wa Kilimahewa anasema akina Mama wa eneo la Kilimahewa wanaipongeza Serikali ya Awamu kwa mageuzi makubwa inayoendelea kuyafanya katika utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo maji, ambapo huko nyuma walikuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta maji, ambayo hayakuwa yakikidhi mahitaji ya nyumbani.

‘’Linapokuja suala la maji, sisi akina Mama tumekuwa tukipata shida sana na kutaabika, lakini tunamshukuru Rais Magufuli na Serikali kwa ujumla kutuletea maji sasa hivi maji yanatoka kwa wakati, yapo safi na salama kwa matumizi’’ alisema Bi. Zubeda.

Bi. Elizabeth Amosi mkazi wa mapoteni Manispaa ya Lindi, anasema akina mama na familia nyingi sasa zina furaha, huduma ya maji imeokoa ndoa za familia nyingi kwani wanaume wengi walikuwa wakigombana na wake zao kutokana na kuchukua muda mrefu wa kwenda na kurudi majumbani wakati wa zoezi la kutafuta maji.

‘’Waume zetu walikuwa na wivu sana ni jambo gumu sana kumwambia mume umetumia masaa 2-3 kwa ajili ya kwenda kutafuta maji katika umbali wa karibu kilometa 2-3 kutoka katika majumba yetu, hayo ndio yalikuwa maisha yetu, lakini kwa sasa shida na matatizo hayo yamekwisha’’ alisema Bi. Elizabeth.

Usimamizi madhubuti wa rasilimali za maji unahitaji ushirikiano wa wananchi na wadau mbalimbali ambao ndio watumia maji na wasimamizi wa kwanza wa rasilimali hizo ikiwa ni mkakati na jitihada za kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji nchini.

MWISHO.