Frank  Mvungi- MAELEZO
Shilingi bilioni 16 zimetumika kujenga  barabara za lami katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano kujenga miundombinu ya kisasa.
 
Akizungumza katika mahojiano maalum mjini Singida, Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini  (TARURA) katika Manispaa hiyo Mhandisi Lambert Bayona amesema ujenzi  huo umetatua changamoto ya ubovu wa barabara katika manispaa hiyo na kuifanya kuwa moja ya maeneo ya kuvutia kwa kuwa na miundombinu ya kisasa ikiwemo  taa za barabarani.
 
“Barabara zenye urefu wa kilomita 9.85 zimejengwa kwa kiwango cha lami zikiwa na njia za waenda kwa miguu, mitaro ya kutiririsha maji,  sambamba na kujengwa kwa stendi ya kisasa ya Misuma iliyogharimu Shilingi bilioni 3 ikiwa na uwezo wa kuhudumia mabasi makubwa zaidi ya 72 kwa wakati mmoja, kuegesha bajaji na bodaboda na maeneo ya kufanyia biashara”, alisisitiza Bayona.
 
Akifafanua, amesema kuwa ujenzi wa stendi hiyo umewezesha mapato ya Halmashauri  kuongezeka kutoka shilingi laki tatu zilizokuwa zikikusanywa awali kabla ya ujenzi huo  hadi shilingi milioni 1.5 kwa sasa baada ya ujenzi huo.
 
Kujengwa kwa stendi hiyo kumeenda sambamba na ujenzi wa stendi ndogo ya daladala inayochangia katika kurahisisha usafirishaji katika Manispaa hiyo.
 
Akizungumzia faida za kujengwa miundombinu hiyo, Bw.  Bayona amesema kuwa imechochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi, kupunguza gharama za usafiri, kuboresha mazingira na kufanya mji huo kuwa wa kisasa ,kupungua kwa ajali, muda wa kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine umepungua na kuongezeka kwa mapato ya halmashauri.
 
Aidha, awamu ya pili ya ujenzi wa barabara za Manispaa hiyo itahusisha kilomita takribani 10 na usanifu wa mradi huo tayari umekamilika.
 
Kwa upande wake mmoja wa wakazi wa Manispaa hiyo, Bi. Maimuna Hamis amesema kujengwa kwa stendi hiyo na barabara hizo kumewawezesha  wananchi  kufanya  shughuli za kiuchumi na kuongeza tija katika uzalishaji.
 
“Naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutujengea barabara za kisasa zenye taa na stendi nzuri hapa Singida”, alisisitiza Bi Maimuna.
 
Naye Meneja wa Stendi hiyo, Bw. Gaudensi Kaziyoba amesema kuwa ujenzi wa stendi umetatua changamoto ya wasafiri kukaa katika maeneo yasiyo na ubora wanaposubiri mabasi kuelekea maeneo mbalimbali mkoani humo,  nje ya mkoa huo na  nchi jirani.
 
Aliongeza kuwa usalama wa abiria na mali zao umeimarishwa katika eneo lote la stendi hali inayowezesha wananchi kufurahia ujenzi wake.
 
Ujenzi wa miundombinu ya barabara, stendi na mingine katika sekta za elimu, afya, maji, nishati na nyingine kunatajwa kuwa kichocheo cha maendeleo katika Mkoa wa Singida na Halmashauri zake zote.
 
……Mwisho….