Ujerumani hapo jana siku ya Jumatatu imeanza hatua ya kuruhusu kufunguliwa kwa maduka kadhaa ya biashara ikiwa ni awamu mpya katika hatua zake za kupambana na janga la kuenea kwa virusi vya Corona.

Hatua hiyo inatekelezwa baada ya shughuli nyingi za kibiashara kufungwa kwa mwezi mmoja. Katika awamu hii mpya maduka yanayoruhusiwa kufunguwa ni yale madogo na yale ya wastani ingawa hatua hiyo inachukuliwa hatua kwa hatua kwa nyakati tofauti na majimbo yote 16.

Katika baadhi ya majimbo, maeneo mengine yatakayofunguliwa ni pamoja na sehemu ambazo wanyama wamehifadhiwa (Zoo). Shule zitafunguliwa kuruhusu watoto wa madarasa ya juu wanaotakiwa kufanya mitihani kujiandaa.

Hatua hiyo itafanyika katika majimbo ya Saxony, Berlin na Brandenburg. Shule nyingine zote zitafunguliwa mwanzoni mwa mwezi Mei.

The post Biashara zafunguliwa Ujerumani, shule mpaka mwezi ujao appeared first on Bongo5.com.