Benki ya dunia imesema uchumi wa bara la Afrika, Kusini mwa jangwa la Sahara utaporomoka kwa kiwango ambacho hakijashuhudiwa tangu miaka 25 iliyopita, kutokana na virusi vya Corona.

Mlipuko wa virusi vya Corona unaozidi kusambaa unatarajiwa kuzisukuma nchi za Afrika,Kusini mwa Jangwa la sahara katika mporomoko wa kiuchumi katika mwaka huu 2020 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25. Huo ni utabiri uliotolewa na benki ya dunia.

Kwa mujibu wa DW, Ripoti ya benki ya dunia kuhusu hali ya kiuchumi barani Afrika imesema kwamba uchumi wa bara hilo utashuka asilimia 2.1 na kufikia asilimia 5.1 kutoka kiwango cha ukuaji cha mwaka jana cha asilimia 2.4.

Aidha mlipuko huu wa virusi vya Corona utazigharimu nchi za ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika dola bilioni 37 hadi dolla bilioni 79 ambayo ni hasara itakayoonekana mwaka huu kufuatia kuvurugwa kwa shughuli nyingi za kibiashara na kiuchumi miongoni mwa sababu nyinginezo.

Bara la Afrika lina alau visa 10,956 vya watu waliothibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona, vifo 562 na waliopona wakiwa ni 1,149 kwa mujibu wa mahesabu yaliyofanywa na shirika la habari la Reuters kwa kuzingatia taarifa zilizokwishatolewa na serikali na data za shirika la afya duniani WHO.

The post Benki ya Dunia: Uchumi wa Afrika kuporomoka kisa Corona  appeared first on Bongo5.com.