BALOZI wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki ameeleza sababu za Serikali ya China katika Jimbo la Guangdong kuwapima Covid-19 kwa lazima Waafrika wanaoishi katika Mji wa Guangzhou nchini humo.

Kairuki pia amefafanua sababu za raia wa Waafrika kutimuliwa kwenye mahoteli na majumba katika mji huo. Alisema baada ya kuona katika mitandao ya kijamii taarifa kuhusu raia wa Afrika kutimuliwa hotelini na kwenye majumba ya wenyeji pamoja na kupimwa Covid-19 kwa lazima, mabalozi wote wa nchi za Afrika waliopo China waliungana na kutaka maelezo kutoka katika mamlaka za juu nchini humo.

Kairuki alisema walifanikiwa kukutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Chen Xiaoding, Jumatatu iliyopita na kupewa ufafanuzi wa kilichowakumba raia wa Afrika nchini humo.

Kwa mujibu wa Balozi Kairuki, Naibu Waziri Chen alitoa sababu tatu zilizosababisha Serikali ya Jimbo la Guangdong kutekeleza upimaji huo wa lazima. Chen aliwaeleza mabalozi hao sababu ya kwanza kuwa miongoni mwa wagonjwa wapya kati ya watu 26 waliopimwa katika jimbo hilo ambao ni wageni kutoka nje, 19 walikuwa wametoka Afrika na ni Waafrika.

Sababu ya pili iliyoelezwa na Chen ni katika kufanya upimaji kwa watu mbalimbali, ilidhihirika kati ya watu 60 waliopimwa ambao hawakuwa na dalili yoyote kama vile kukohoa au homa, 57 walikutwa na maambukizi ya Covid-19 na wote ni waafrika.

Kairuki alisema sababu ya tatu waliyopewa ni kwamba katika muda wa wiki mbili zilizopita, China ilifanikiwa kudhibiti maambukizi ya ndani, lakini katika siku za hivi karibuni kumekuwa na watu wachache walioambukizwa, na ikabainika kuwa katika Jimbo la Guangdong, kati ya maambukizi 15 ya ndani, 13 ni watu wa mataifa ya Afrika.

Sababu hizi tatu ndizo zilizosababisha serikali kufanya utafiti ili kuona watu hawa ambao wameathirika wamekutana na watu wangapi ili washughulike na watu wangapi, kupitia utafiti huo, walibaini watu hawa walikutana na watu wengi sana,” alisema Balozi Kairuki.

Kutokana na mnyororo mrefu wa wagonjwa hao kukutana na watu wengine, ndipo serikali nchini humo iliona haja ya kufanya upimaji wa lazima kwa Waafrika ili kudhibiti mlipuko ndani ya jamii na ndipo upimaji ukaanza. Kairuki alisema baada ya upimaji huo kuanza, changamoto nazo zikajitokeza kwa sababu maelezo sahihi hayakutolewa mapema jambo ambalo Naibu Waziri Chen alikiri.

Pamoja na kukiri kuwepo kwa mapungufu hayo, Chen aliwahakikishia mabalozi hao kuwa Sera ya China hairidhii masuala ya ubaguzi wa aina yoyote, isitoshe China ni rafiki wa kweli na rafiki wa majira yote wa Tanzania na mataifa yote ya Afrika. Kuhusu raia wa Afrika kutimuliwa hotelini na kwenye majumba, Balozi Kairuki alisema baadhi ya Waafrika hao hawakuwa na viza za kuishi nchini humo na wengine viza zao zilikuwa zimeisha muda wa matumizi.

Alisema baada ya upimaji wa lazima wa Covid-19 kuanza, wamiliki wa hoteli na majumba waliogopa kukumbana na mkono wa serikali kwa kuwahifadhi wageni kinyume cha sheria, hivyo wakaamua kuwaondoa.

Katika sakata hilo, Balozi Kairuki alisema hakuna Mtanzania hata mmoja aliyeathirika, wote wako salama, wengi wao wameshapimwa kupitia upimaji wa lazima na wawili tu ndiyo walikutwa na maambukizi ya Covid-19.

The post Balozi Kairuki aeleza sababu ya Waafrika kupimwa corona kwa lazima China appeared first on Bongo5.com.