SALVATORY NTANDU
Mkazi wa kijiji cha Mwakitolyo namba 2 Mkoani Shinyanga, Mussa Jackson (25) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa anaugua ugonjwa uanaosababishwa na virusi vya Corona.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba alisema Musaa alimpigia   simu na kumdanganya Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee, Walemavu na Watoto Ummy Mwalimu kuwa ana ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Kamanda Magiligimba alisema kuwa baada ya Musaa kutoa taarifa hizo kwa Waziri, timu ya madaktari inayotoa huduma eneo la halmashauri ya wilaya ya shinyanga vijijini kuhusiana na ugonjwa wa covid 19 ilifika eneo la kijiji cha mwakitolyo namba 02 ili kutoa huduma kwa mtu huyo lakini mtu huyo alizima simu yake na kusababisha timu hiyo ya madaktari kushindwa kumpata hivyo kusababisha taharuki.

Amefafanua kuwa mnamo Aprili 15 majira ya saa moja asubuhi kikosi kazi cha askari wa makosa ya kimtandao  walifika eneo la mwakitolyo namba 02 na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa anaendelea na shughuli zake za uchimbaji katika  eneo hilo.

“Baada ya kukamatwa Mussa alifikishwa katika  zahanati ya kijiji cha mwakitolyo namba 02, ambapo timu ya madaktari walimfanyia vipimo vya awali vya magonjwa nyemelezi yanayoashiria kuwepo kwa uwezekano wa mtu kuwa na ugonjwa wa covid 19 lakini hakuwa na dalili za magonjwa hayo,”alisema Kamanda Magiligimba.

Ameongeza kuwa baada ya kuhojiwa mtuhumiwa amekiri kutoa taarifa hiyo na kwamba baadaye aliamua  kuiharibu laini yake ya simu kwa kuivunjavunja ili asiweze kupatikana.

Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa wananchi kuacha masihara juu ya ugonjwa covid 19 na mtu yeyote atakayetoa taarifa za uongo juu ugonjwa huo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mwisho.