Na John Walter-Manyara
Wakina mama zaidi ya 2,700 katika mkoa wa Manyara na Kilimanjaro wameweza kunufaika na mradi wa kutokomeza vifo vya akina mama wajawazito na watoto kupitia shirika la Pharm Access katika  mradi wa Momcare.

Akizungumza na Mtandao huu meneja wa mradi  Pharm Access Foundation Dr.Johnson Mali amesema walionufaika ni wakina mama kutoka katika vituo 215 wanavyovihudumia katika mikoa ya Manyara na Kilimanjaro.

Mradi wa Momcare ulianzishwa mwaka jana chini ya ufadhili kutoka nchini Japan  kwa ushirikiano na mashirika ya kimataifa kwa  kugharamia mafunzo ya afya na usafiri kwa akina mama wajawazito wanaokaribia kujifungua.

Dr. Mali amesema kwa zaidi ya Mhongo mmoja sasa shirika limekuwa likiendesha miradi mbalimbali inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi hapa nchini kwa ufadhili wa serikali ya Uholanzi.

Aidha kwa kipindi cha miaka mitano 2014-2019 Pharm Access kwa kushirikiana na shirika la Bima ya afya –NHIF na serikali za mikoa,walianzisha na kuendesha mradi wa mfuko wa afya ya jamii uliyoboreshwa (Ichf) katika mikoa ya Kilimanjaro na Manyara ambapo zaidi ya kaya laki moja ziliandikishwa na kupata huduma za matibabu vituoni ambapo kwa sasa model ya Ichf imechukuliwa na serikali kuu na inatumika nchi nzima.

Kwa upande mwingine Shirika la Pharm Access kuanzia May 2019 lilianza kufanya mradi mwingine unaoitwa “Safari salama” ya mama Mjamzito au Momcare ambao unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma bora za uzazi kwa mama mjamzito kuanzia mimba hata baada ya kujifungua ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Meneja wa mradi, amesema kupitia mradi huo akina mama wajawazito huhamasishwa kuanza kliniki mapema na vituo hulipwa fedha ambazo husaidia kuboresha huduma huku wakina mama na familia zao wakilipiwa kujiunga na mfuko wa iCHF bure.

Amesema katika miradi yao yote, moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele ni uboreshaji wa huduma zinazotolewa kwenye vituo vya kutolea matibabu (Quality Improvement) na kwamba wanafanya hivyo ili huduma ziweze kutolewa katika hali ambayo haitarishi usalama wa mgonjwa na mtoa huduma.

“Hili limekuwa likifanyika kupitia kufanya mafunzo kwa watumishi vituoni,kutoa miongozo (treatment guidelines) na wakati mwingine vifaa tiba (Medical equipment)” ilieleza taarifa ya Dr. Mali.

Katibu tawala mkoa wa Manyara amelishukuru shirika hilo kwa kuisaidia serikali katika kuboresha afya za wakina mama kwa kuwapatia vifaa vinavyowaasidia pindi wanapokwenda katika vituo vya afya kujifungua na kuwataka waendelee kutoa.