Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametangaza mpango wa hatua za kiuchumi wa dola bilioni 26 ili  kuupiga jeki uchumi  wa nchi hiyo na kusaidia jamii masikini zilizoathirika na janga la virusi vya corona. 

Akilihutubia taifa usiku wa kuamkia leo Ramaphosa amesema athari za ugonjwa wa COVID-19 zinahitaji bajeti maalum na mpango huo wa kihistoria utasaidia uchumi wa taifa hilo la watu milioni 58. 

Ramaphosa amesema Afrika Kusini sasa inaingia kwenye awamu ya pili ya kushughulikia kadhia ya corona kwa kuufufua uchumi ambao kuanguka kwake kumevuruga uzalishaji na nafasi za ajira. 

Rais huyo amesema kiasi dola bilioni 2.3 zitaelekezwa kutoa msaada wa fedha kwa jamii masikini huku vifurushi 250,000 vya chakula vitasambazwa kwa raia walio na mahitaji katika kipindi cha wiki mbili zinazokuja. 

Nchini Afrika Kusini kunaripotiwa visa 3,465 vya maambukizi ya virusi vya Corona yaliyothibitishwa, na watu 58 wamefariki  kwa ugonjwa huo.

Credit:DW