Viongozi wawili wanaohasimiana nchini Afghanistan wanajiandaa kuapishwa leo, baada ya kushindwa kufikia makubaliano kuhusu Taliban.

Hatua hiyo imeszusha hofu kwa demokrasia dhaifu ya Afghanistan, wakati ambapo Marekani inajiandaa kuondoka nchini humo baada ya kufikia makubaliano na Taliban mwezi uliopita.

Uchaguzi ulifanyika mwezi Septemba, lakini rais aliyeko madarakani Ashraf Ghani alitangazwa kuwa mshindi kwa kipindi cha pili mwezi Februari baada ya kuwepo malalamiko ya udanganyifu katika uchaguzi, hali iliyosababisha hasira kwa kiongozi wa kisiasa wa ngazi ya juu nchini Afghanistan, Abdullah Abdullah ambaye aliapa kuunda serikali yake mwenyewe.

Imeripotiwa kuwa mazungumzo ya mwisho yaliendelea hadi usiku wa jana, wakati ambapo pande hizo mbili zikitafuta kufikia makubaliano. Lakini hadi leo asubuhi kulikuwa na dalili ndogo za suluhisho kupatikana na msemaji wa Abdullah, Faraidoon amesema sherehe za kuapishwa kiongozi wake zitaendelea kama zilivyopangwa.