MSANII wa muziki Raia wa Kenya, Tanasha Donna amefunguka sakata la kuachana na mzazi mwenzake ambaye pia ni staa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz na kueleza kwa sasa hayupo tayari tena kuwa kwenye mahusiano.

Kupitia ujumbe ambao ameuweka kwenye Insta Stories amesema kuwa haoni sababu ya kulipa ubaya kwa yale aliyotendewa kwani kwa siku za hivi karibuni amepata baraka nyingi sana.

 
“Pale watu wanapokukosea usiwakosee na wewe kwa ubaya pia, unaweza kupambana kwa mabaya kwa mazuri. Utalala vizuri ukijua wewe ulikuwa halisi na sio bandia, ukisubiri walipwe mabaya yao,” amesema Tanasha.

Amesema kuwa baraka ambazo amekuwa akizipokea kwa hizi wiki hizi mbili ni za ajabu sana, wasanii mbalimbali wa kimataifa wamekuwa wakimtafuta kwa ajili ya kufanya naye kazi na anafahamu kuwa Mungu hakumsahau.


Pia, ameeleza kuwa kwa sasa wanaume wengi maarufu wamekuwa wakimsumbua wakitaka kuwa naye kimapenzi baada ya kusikia ameachana na Diamond lakini kwa sasa hayupo tayari kuwa kwenye mahusiano yoyote yale.