Na Peter Haule WFM, Dodoma
Serikali imezitaka Taasisi zote za Manunuzi ambazo hazijajiunga katika Mfumo wa Ununuzi ya Umma kwa njia ya Mtandao (e-Procurement System) ujulikanao kama TANePS kufanya hivyo kinyume na hapo zitakuwa zimejipotezea nafasi za kushiriki katika Zabuni zinazojitokeza.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Balozi Dkt. Matern Lumbanga, wakati wa Ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa PPRA, jijini Dodoma.

Balozi Lumbanga amewataka Watumishi wa  PPRA, kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu matumizi ya mfumo wa TANePS kuhakikisha kwamba taasisi zote za umma ambazo hazijajiunga na mfumo zinaunganishwa kwenye mfumo na kuanza kuutumia katika manunuzi yake kabla ya kufunga mwaka huu wa fedha 2019/2020.

”Ni imani yangu kuwa mfumo huu utakuwa mwarobaini wa changamoto ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwenye ununuzi ya umma kama vile, michakato ya zabuni kutumia muda mrefu na gharama kubwa, kukosekana ushindani, uwazi na usawa kwenye michakato ya zabuni  na pia bei kubwa za bidhaa na huduma ikilinganishwa na bei halisi ya soko”, alieleza Balozi Lumbanga.

Pia Dkt. Lumbanga amewakumbusha watumishi wa PPRA kuzingatia kanuni zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya juu ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Corona ambao ni tishio kwa Dunia.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo, alisema kuwa Taasisi Nunuzi na Wazabuni, wanaendelea kupatiwa mafunzo ya jinsi ya kuutumia na kujiunga kwenye mfumo wa TANePS na hadi sasa Taasisi Nunuzi 511 kati ya 540 zimepata mafunzo na zimeanza kuutumia mfumo huo.

Mhandisi Kapongo alieleza kuwa, Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa PPRA ni cha tatu tangu kuanza kwa Baraza hilo la Wafanyakazi wa PPRA na ni kikao cha pili katika mwaka huu wa fedha wa 2019/20.

Alisema kuwa Mamlaka imejiwekea utaratibu wa kufanya vikao viwili ya Baraza la Wafanyakazi katika kila mwaka wa fedha ili kujadili kwa pamoja njia za kuboresha mafanikio yanayokuwa yamepatikana na njia za kutatua changamoto zinazoikabili Mamlaka.

Mhandisi Kapongo alisema kuwa katika Kikao cha Baraza hilo la Watumishi watapokea, kujadili na kupitisha taarifa ya nusu mwaka ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2019/2020, na kujadili na kupitisha Bajeti inayopendekezwa ya mwaka 2020/2021.