Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali inaendelea kufanya tathmini, ili kuhakikisha inazuia virusi vya corona havienei kwa kiasi kikubwa nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na Mawaziri na Makatibu Wakuu wa wizara mbalimbali katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma.

 Alisema serikali imeunda Kamati tatu kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya corona ambayo ni ile ya Kitaifa inayoongozwa na yeye mwenyewe na itahusisha baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu wa wizara na Msemaji Mkuu wa Serikali.

 Ameitaja kamati ya pili kuwa ni ile ya Makatibu Wakuu  kutoka Wizara mbalimbali na itaongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na kamati ya tatu ni ya Kikosi Kazi cha Taifa ambayo itaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto huku wajumbe wake wakiwa ni wataalamu akiwemo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 
Awali akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alisema kuwa katika kipindi cha saa 24 zilizopita, zaidi ya watu laki mbili na tisini elfu duniani wamebainika kuambukizwa virusi vya corona na kati yao 12,784 wamefariki dunia.

 Aidha, Barani Afrika watu 736 wamebainika kuambukizwa virusi hivyo vya corona, huku Ishirini wakifariki dunia katika kipindi hicho cha saa 24 zilizopita.