Rais Magufuli amesema uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu hautaahirishwa licha ya kuwepo kwa mlipuko wa virusi vya corona (Covid-19).

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Machi 26, 2020 wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ripoti ya Taasisi ya Kuzuna Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

“Sisi tunaendelea kukutana, ndiyo maana hata Bunge linaendelea na vikao vyake, hata huko kwenye nchi zilizoathirika kabisa, mamilioni ya watu wamekufa kwa corona, bado mabunge yao na mabaraza ya madiwani yanakutana. Kazi lazima ziendelee.

“Na uchaguzi tutafanya, wapo wanaofikiri kwamba tutaahirisha, unafikiri nani anataka kukaa kwenye maofisi haya muda wote huo,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameeleza kushangazwa na mwandishi mmoja kuandika habari kwamba “Baraza la madiwani lafanya mkutano licha ya corona” na kuhoji kama mikutano ya aina hiyo imezuiwa.

Amesisitiza kwamba kazi lazima ziendelee kufanyika licha ya uwepo wa virusi hivyo na mikutano ya baraza la madiwani, Bunge na hata ile anayoifanya yeye itaendelea kufanyika kwa sababu ni sehemu ya kazi zao.