Miaka minane tangu afariki mwigizaji Steven Kanumba, familia yaingia katika mgogoro mzito wa kugombea mali.

Kanumba ambaye alipata umaarufu ndani na nje ya nchi kwa uigizaji alifariki Aprili mwaka 2012.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe aliteua kamati ya kusimamia na kulinda kazi za wasanii, ambapo wanufaika wa kwanza walikuwa marehemu King Majuto na Steven Kanumba kwa kubanwa kampuni walizokuwa wakifanya nazo kazi ya matangazo kuzilipa familia zao kifuta jasho.

Kutokana na hatua hiyo, mwaka jana mama Kanumba alianza kupokea fedha kutoka kwa baadhi ya kampuni hizo.

Madai yaliyotolewa na familia ya upande wa baba wa Kanumba yanaeleza kuwa mama huyo hakumgawia mzazi mwenzake huyo hata kitu kimoja ikiwamo fedha na mali nyingine licha ya kuwa mmoja wa warithi.

Akizungumza na Mwananchi, Mjanael Kanumba aliyejitambulisha kama ndugu yake Kanumba waliochangia baba alisema kuwa katika mgao wa fedha na mali za ndugu yao huyo, baba yao hakupata kitu hata kimoja.


“Siku za nyuma ilikuwa ngumu kufuatilia kwa sababu mzee hali yake siyo nzuri kiafya na mimi nilikuwa namalizia masomo, lakini sasa nina nafasi nitafuatilia kuhakikisha baba anapata jasho la kijana wake.

“Safari hii nina muda nitafuatilia mpaka mwisho kuona na baba naye anapata haki hiyo hata kwa kwenda mahakamani, kwa kuwa hata katika wosia anatambulika kama ni mmoja wa warithi,”alisema Mjanael Kanumba.

Kwa upande wa baba wa mwigizaji huyo , Charles Kanumba alisema alipata taarifa kuwa mama Kanumba ameuza kila kitu, na fedha za kifuta jasho za kampuni mbalimbali zilizokuwa zikifanya kazi na kijana wetu kachukua.

“Sasa nawatuma vijana wangu wanisaidie kupambana na mimi angalau nipate mgao wa Startime, ambao nasikia utatoka hivi karibuni,”alisema.

Wakizungumzia sakata hilo Bodi ya Filamu kupitia Kaimu Katibu Mtendaji, Dk Kiagho Kilonzo, ambaye pia ndio katibu wa kamati ya wanasheria iliyoundwa na serikali, alikiri kupokea malalamiko hayo ambayo alieleza kuwa tayari kuyafikisha kwenye kamati.

Wakati Mwenyekiti wa kamati hiyo, Nsangizyo Zilahulula, alisema tayari kamati imeshaanza kushughulikia suala hilo ikiwemo kuwa na vikao vinavyohusisha pande mbili ya wazazi hao wawili yaani mama na baba Kanumbai

Kwa upande wa Startimes kupitia mwanasheria wao, alikiri kuwahi kuitwa na kamati kwa ajili ya malalamiko ya upande wa baba Kanumba na kueleza kuwa wasingependa kuliongelea kiundani suala hilo kwa kuwa bado lipo katika ngazi ya majadiliano na kamati.

Naye Frola Mutegoa ambaye ni mama mzazi wa Kanumba alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo, alisema amechoshwa na malalamiko hayo na kuwataka wahusika waende mahakamani.

“Kama ni mtoto nimemlea mwenyewe, nimehangaika kufuatilia haki zake mwenyewe, leo iweje watu waone hela inatoka ndio wajitokeze, acha tukutane mahakamani itajulikana nani mwenye haki,”alisema mama huyo.

Alisema pia hawakuoana alikuwa ni mchepuko wake na kubahatika kumpata kijana huyo, sasa anashangaa imekuwa nongwa kila siku analalamikia mgao ilihali anajua hakumlea wala kumuhudumia.

“Sioni ulazima wa yeye kunufaika na mali za mtoto ambaye hakumtunza alipokuwa mdogo, iweje amkumbuke baada ya kufa na kusikia kuna kifuta jasho,”alisema.