Maambukizi ya kirusi cha corona yamepindukia 142,000 nchini Marekani na kulifanya taifa hilo kuongoza duniani, huku waliopoteza maisha wakipindukia 2,500.

Katika jimbo la New York pekee, watu zaidi ya 1,000 wameripotiwa kufa, ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu mgonjwa wa mwanzo kugundulika kwenye jimbo hilo.

Kufikia jioni ya jana, eneo la mjini la jimbo hilo lilitangaza kuwa vifo vimefikia 776, huku miji mingine ikitangaza vifo 250, na hivyo kuifanya idadi kamili ya waliopoteza maisha kwa ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na kirusi hicho kufikia 1,026.

Hayo yanakuja wakati Rais Donald Trump akitangaza kwamba huenda vifo vyote vitavyotokana na kirusi hicho vikapindukia 100,000 nchini Marekani. Trump ameongeza muda wa watu kujitenga ili kuepuka maambukizi mapya hadi tarehe 30 mwezi Aprili.

Muda wa awali uliowekwa ulikuwa wa wiki mbili, ambao unamalizika leo.