Na  Mbaraka Kambona,
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imeiagiza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki Maendeleo kuandaa mapendekezo yatakayosaidia kuanzishwa kwa mchakato wa  kutungwa kwa sheria ya kulinda haki za mtumiaji wa huduma za mifumo ya kimtandao na kuyawasilisha kwa kamati hiyo ili waweze kushawishi bunge na mamlaka nyingine husika ili sheria hiyo iweze kutungwa.

Maelekezo hayo yalitolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Emmanuel Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini kufuatia mada kuhusu haki za binadamu na Mitandao iliyowasilishwa vyema na Mwenyekiti wa Bodi ya Haki Maendeleo, Dk. Abdallah Mrindoko katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki Maendeleo kwa wabunge wa kamati hiyo Iliyofanyika Mkoani Morogoro Machi 16, 2020.

Akiongea baada ya kuwasilishwa kwa mada hiyo, Mwakasaka alisema kuwa kuna haja ya kuwa na sheria itakayolinda usiri wa taarifa za mtumiaji wa huduma zinazotumia mifumo ya kimtandao kwa kuzingatia kuwa mifumo hii inachakata taarifa za mtumiaji na kuzisambaza jambo ambalo linaibua haja ya kutungwa kwa sheria hiyo.

Mapema wakati akitoa mada hiyo, Dk. Mrindoko alitaja changamoto kubwa inayowakumba watumiaji katika kipindi hiki cha maendeleo ya teknolojia ya mtandao ni uwepo wa taasisi nyingi zinazojihusisha na utunzaji na uchakataji wa taarifa katika mfumo wa kidijitali bila kuwepo na sheria ya kulinda haki hizo za mtumiaji.

Dk. Mrindoko aliongeza kuwa ili thamani ya matumizi ya mitandao iweze kutambulika vizuri ni muhimu kuwa na sera na sheria itakayosimamia ulinzi wa haki  za mtumiaji nchini.

Aliendelea kusisitiza  kwamba mapinduzi ya huduma ya kifedha kwa njia ya mitandao ya simu imeibua changamoto nyingi zinazohusiana na ulinzi wa haki za mtumiaji, akisema kuwa jukwaa hili limeleteleza muingiliano kati ya kampuni za mawasiliano na taasisi za kifedha, mazingira ambayo yameibua hoja ya kuwepo sheria ya kusimamia masuala hayo.

“Mazingira yaliyopo sasa yametengeneza ombwe la kisheria kufuatia kuwepo kwa pande  mbili ambazo ni kampuni za simu na taasisi za kifedha zinazosimamia masuala ya kifedha mitandaoni ambapo kila mmoja ana mipaka yake kiutendaji”, alisema Dk Mrindoko

“Wakati matumizi ya simu katika kutuma na kupokea pesa kumepelekea ukuaji na urahisi wa mzunguko wa masuala ya kifedha, bado kuna changamoto nyingi zinazohusu mustakabali wa mtumiaji ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi, aliongeza Dk. Mrindoko

Aidha,  alieleza kuwa maendeleo katika matibabu ya afya ya kimtandao na kitambulisho cha uraia vimeleteleza maswali mengi kuhusiana na ulinzi na usiri wa taarifa za mtumiaji, akipendekeza kuwa mambo yote haya inabidi yawe katika mfumo mmoja ambao utalinda usiri na taarifa za mtumiaji. 

Akichangia majadiliano katika warsha hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome alikiri kuwa ni muhimu kuwa na sheria zinazolinda usiri na taarifa za mtumiaji huku akisema kuwa mchakato wa kutunga sheria hiyo hivi sasa ipo katika mchakato wa kutungwa ili iweze kutumika.