SALVATORY NTANDU
Jamii Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga imeaswa Kutowanyanyapaa na Kuwatenga Wagonjwa wa Kifua Kikuu wanaoendelea  na Matibabu katika Zahanati na Vituo vya Afya  mbalimbali kwa kuwahusisha na  Ugonjwa wa Korona ambao dalili zake zinashabihiana jambo ambalo linaweza kusababisha Wagonjwa wengi kukata Tamaa na kuacha ufuasi wa matibabu .

Hayo yalibainishwa Machi 24 na Anisia Mrigo Afisa Mradi wa Kifua Kikuu kutoka shirika lisilo la Kiserikali la Shidepha+ wakati akizungumza na Waandishi wa habari Mjini Kahama katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya kifua kikuu Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 24 yaliyokwenda sambamba na utoaji elimu kwa Umma kupitia vyombo vya habari kuhusiana na  ugonjwa huo.

Alisema katika Jamii kumeanza kujitokeza vitendo vya unyanyapaa kwa wagonjwa wa kifua kikuu kutoka  kwa  baadhi ya watu wasiokuwa na elimu sahihi juu ya ugonjwa wa Corona wameanza kuwatenga wagonjwa wa kifua kikuu kwa kuwahusisha kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo jambo ambalo linawezea kusababisha kuongezeka wa maambukizi mapya ya kifua kikuu kwenye jamii.

“Endapo tutawatenga wagonjwa wa kifua kikuu katika jami zetu tunaweza kusababisha wakapoteza maisha kwani wapo baadhi ya watu wameanza kuwanyima chakula,kwa madai ya kuwa dalili za ugonjwa wa Corona zinafanana na ugonjwa wa kifua kikuu”,alisema Mrigo.

Awali akizungumzia Suala hilo Naibu Mkurugenzi Miradi wa Shidepha+  Shekha Nassoro ni alisema kuwa  Wagonjwa wa Kifua Kikuu bado wapo kwenye jamii na wanapaswa kusaidiwa kwa kupatiwa msaada wa matibabu na kutoa rai kwa wananchi kuachana na vitendo hivyo ambayo sio vya kiungwana.

“Katika jamii zetu kama kunamgonjwa wa Kifua kikuu toeni taarifa kupitia mawasiliano yafuatayo bure kwa kupiga *152*05*06# katika kipindi hiki ili kuwasaidia pindi wanapopata matatizo ya kiafya”,alisema Nassoro.

Nae  Meneja Mradi wa Kifua Kikuu kutoka Shirika lisilo la kiserikali la  Shidepha+  Elneus Mwinuka alisema kuwa tangu waanze kutekeleza mradi wa kupambana na kutokomeza kifua kikuu katika mikoa ya Geita na Shinyanga umeweza kuleta matokea chanya kwa kufanikiwa kuwafikia wagonjwa wengi ikilinganishwa hapo awali ambapo ilikuwa ni vigumu wagonjwa wa kifua kikuu kujitokeza hadharani.

“Zamani ilikuwa ni ngumu kwa wagonjwa wa kifua kikuu kujitokeza kupima afya zao wengi wao walikuwa wanaamini kuwa kifua kikuu kinasababishwa na imani za kishirikina jambo ambalo halina ukweli wowote,”alisema Mwinuka.

Kwa upande wake Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma kutoka Hospitali ya Mji wa Kahama Mkoani Shinyanga Mariamu Mabanga amesema maambukizi ya Kifua Kikuu yapo juu katika jamii ambapo kwa mpaka sasa kuanzia Januari hadi sasa wanawagonjwa 200 ambapo wagonjwa wengi wanatoka katika mikoa ya jirani kama vile Tabora na Geita na kuwaasa wananchi kutowanyanyapaa wagonjwa waliothibitika kuwa na ungonjwa huo kwa muda mrefu.

Mwisho.