Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma
Mbunge wa jimbo la Kawe jijini  Dar Es  Salaam Mhe.Halima  Mdee ameishauri  Serikali kufanya mchakato wa kupima Corona wabunge wote na watakaobainika wawekwe karantini.

Mhe.Mdee amesema hayo leo Machi 31,2020 bungeni jijini Dodoma ambapo amebainisha kuwa inatakiwa kila mbunge apimwe homa ya Mapafu inayosababishwa na virusi vya corona[COVID -19]na akibainika  na maambukizi ya  virusi hivyo atengwe eneo maalum[karantini] na wale watakaobainika kutokuwa na maambukizi waendelee na mkutano ili kujadili bajeti kuu ya serikali ikiwa ni mkutano wa Mwisho kuelekea uchaguzi mkuu.

“Leo wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi wote,kwa nini tusipime wote atakayebainika ana virusi apelekwe karantini na akiwa salama abaki hapa kujadili mambo ya msingi kwa mstakabali wa taifa letu  maana ni mkutano wa mwisho”amesema.

Naye,Mbunge wa   Iringa Mjini  Mch.Peter  Msigwa ameiomba serikali kuja na mpango wa pamoja katika kujadili katika mapambano ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu inayosababishwa na virusi vya corona[COVID-19].

Spika wa bunge la  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Job Ndugai amesema katika mkutano wa bunge  la bajeti  ni vyema majadiliano ya pande zote mbili yakazingatiwa huku akitoa wito kwa wabunge kusikilizana na kuelekeza zaidi kwenye bajeti kwani ni mkutano wa Mwisho ambapo bunge litavunjwa kuelekea uchaguzi mkuu  2020.

“Kikao ni chetu kisiwe cha upande mmoja au watu wachache hata kidogo kwa hiyo natoa wito kusikilizana kwa pande zote mbili na ni vyema zaidi mbunge ukajielekeza kwenye bajeti kuliko ukasimama na yako tu ni muhimu sana kuzingatia muda”amesma.

Katika hatua nyingine Mhe.Ndugai ametoa maelekezo kwa serikali kuandaa majibu haraka iwezekanavyo juu ya Hoja Za Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali[CAG] zilizowasilishwa hivi karibuni kwa  Mhe.Rais .